Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TCRA yaburuta 13 kortini kwa kuchapisha uongo

10760 Pic+tra TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewaburuta mahakamani watu 13 kwa tuhuma za makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa zaidi ya Sh154 milioni.

Pia, watu hao wanadaiwa kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo kwa njia ya kielektroniki.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Boniface Maombe, David Luvanda, Moshi Sungura, Amos Bosco, Lule Kadenge, Jofrey Kapangamwaka, William Nturo, Regius Mauka, Collins Mwang’omolan, Francis Kapalata, Kasonde Kapela, Enock Mwandaji na Pascal Kiatu.

Wakili mkuu wa Serikali, Tumain Kweka aliwasomea mashtaka ya uhujumu uchumi namba 58/2018 jana mbele ya Hakimu Kelvin Mhina wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Aliiambia mahakama kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa mashtaka ya kula njama, kuchapisha taarifa za uongo na mawili ya kusambaza taarifa za uongo na shtaka moja la utakatishaji wa fedha.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa maelezo hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo, wala kutoa dhamana hadi Mahakama Kuu.

Hata hivyo, shtaka la utakatishaji wa fedha ni miongoni kwa mashtaka yasiyo na dhamana.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, iliahirishwa hadi Agosti 21.

Jopo la mawakili wa Serikali linaundwa na Kweka, Kishenyi Mutalemwa, Nassoro Katuga, Patrick Mwita, Faraji Nguka na mwanasheria wa TCRA, Johannes Karungura.

Chanzo: mwananchi.co.tz