TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha,
imeweza kuokoa fedha zaidi ya sh, bilioni 4.2, kutoka kampuni
mbalimbali za utalii, ikiwemo ya uwindaji ya Otterlo Business
Corporation (OBC),vyama vya ushirika, Vikoba na Saccos, katika
kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu.
Aidha fedha hizo ni pamoja na kodi za serikali, fedha za watu binafsi,
mikopo umiza na fedha za wakulima na wajasiriamali.
Kwamujibu wa taraifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Jijini
hapa na Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, James Ruge alisema
sh,bilioni 3.5 zimelipwa na kampuni ya kitalii ya OBC,sh, milioni 60
zimelipwa na kampuni ya ANICROP Services ambazo ni kodi ya serikali
zilizokwepwa kulipwa na makampuni hayo kwa nyakati tofauti kati ya
mwaka 2018/2020.
Alisema kati ya fedha hizo pia zaidi ya sh, milioni 28.9 ni kodi na
mikopo ya serikali iliyokwepwa kurejeshwa na kufanyiwa ubadhirifu na
wananchi pamoja na watendaji mbalimbali wa serikali katika nyakati
tofauti.
Aidha kutoka vyama vya Ushirika jummla ya sh, milioni 98.9 za Chama
Kikuu cha Ushirika cha Arusha Cooperation Union (ACU) zilizokuwa
zimefanyiwa ubadhirifu baada ya mali za chama hicho kuuzwa kwa watu
wasio waaminifu na zaidi ya sh, milioni 4.3 zililipwa na Bodi ya
Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), pamoja na sh, milioni 8 ni
michango ya wanachama wa mabaraza ya wafugaji, iliyofanyiwa ubadhirifu
na viongozi wao.
“Fedha zingine tumeziokoa kutoka VIKOBA na SACCOS ambazo ni zaidi ya
sh, milioni 86.5 ambazo ni mikopo mbalimbali iliyokuwa haijarejeshwa
kw amuda mrefu kinyume na taratibu,”.
Ruge alisema fedha zingine zimetoka kwa watu binafsi na mikopo
umiza, ambazo ni zaidi ya sh, milioni 194 zilizokuwa za madai ya watu
binafsi mbalimbali na mikopo iliyokuwa imetolewa kwa riba kubwa na
Taasisi za kifedha IVOJ Micro Credit Co Ltd ya jijini Arusha na Rhobi
Credit Co Ltd ya Karatu.
Pia madai ya wakulima na wajasiriamali wameokoa zaidi ya sh, milioni
289.2 zilizokuwa zilipwe na kampuni ya Kijenge Animal Products kwa
wakulima waliouzia kiwanda hicho bidhaa za kilimo,lakini hawakulipwa
kwa muda mrefu.
“Pia zaidi ya sh, milioni 5.9 ni fedha za wakulima waliouza mazao yao
kwa kampuni ya TBL na kampuni moja ya mbegu iliyopo wilayani Monduli
bila kupewa malipo yao,”.