Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sukari tani 23 yanaswa ikiuzwa bei ya ulanguzi

SUKARII.webp Sukari tani 23 yanaswa ikiuzwa bei ya ulanguzi

Mon, 27 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BODI ya Sukari Tanzania (SBT), imekamata shehena ya sukari zaidi ya tani 23.

Kiasi hichi kinahusisha sukari iliyoagizwa nje ya nchi na ya ndani, ikiuzwa kwa bei ya ulanguzi, tofauti na bei elekezi iliyotangazwa na serikali wiki iliyopita.

Walionaswa na sukari hiyo walikuwa wameificha kwenye baadhi ya maghala, wakiwamo wafanyabiashara wakubwa katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Katika operesheni hiyo maalum iliyoendeshwa jana kwa usiri na maofisa wa bodi hiyo wakishirikiana na askari kanzu wa Jeshi la Polisi, Nipashe ilishuhudia sukari hiyo ikizuiwa isiendelee kutumika hadi hapo serikali itakapotoa maelekezo mengine.

Ofisa Mwandamizi wa Udhibiti wa SBT, Faustine Mgimba, akizungumza baada ya operesheni hiyo, alisema wamebaini sukari hiyo ilikuwa ikiuza kwa walaji kwa bei ya rejareja ya Sh. 3,400 tofauti na bei elekezi ya Sh. 2,700 kwa kilogramu moja kwa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Pwani, Tanga na Morogoro.

Wafanyabiashara hao, walitumia pia ujanja wa kuuza mfuko mmoja wa sukari wa kilogramu 50 kwa Sh. 135,000 ambayo ni tofauti na bei elekezi ya Sh. 128,000.

Zaidi Mgimba alieleza: “Tumegundua kwamba changamoto kubwa katika maduka mengi, wafanyabiashara wameshindwa kuwa wa kweli, wengi wao hawajaweza kuonyesha nyaraka za uagizaji sukari kutoka kwa mawakala wakubwa ili kuthibitisha uagizwaji wake.

“Na baadhi yao wameficha kiasi kikubwa cha sukari ili kuuza kwa bei kubwa, kitu ambacho ni kuwakandamiza walaji.”

Katika operesheni hiyo, maofisa wa SBT pia walikamata gari dogo aina ya Pick Up iliyokuwa ikitorosha sukari hiyo ili kuepuka mkono wa dola.

Aprili 23, mwaka huu, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alitangaza bei elekezi ya sukari kwa kila mkoa nchini, huku akiwaonya watakaobainika kuuza kinyume cha utaratibu huo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwamo kunyang’anywa leseni za biashara.

Sheria ya Sukari Na. 26 ya Mwaka 2001 chini ya kifungu cha 11A, inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya kilimo, kutangaza bei ya ukomo wa juu ya sukari.

Waziri Hasunga alinukuliwa akisema bei hiyo elekezi imepangwa kwa kuzingatia gharama zote za uagizaji wa sukari ya kuziba pengo zinazotumiwa na wazalishaji kuagiza sukari kutoka nje ya nchi na umbali wa kila eneo.

Hata hivyo, baadhi ya maofisa mauzo na ugavi katika maduka makubwa yaliyonaswa na sukari hiyo, walidai wameagiza sukari kutoka jijini Dar es Salaam kwa wakala mmoja.

Wakati operesheni hiyo ikiendelea, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alikwenda katika Kiwanda cha Sukari cha TPC, ambapo alieleza kuwa serikali imeagiza tani 40,000 kwa ajili ya kuongeza usambazaji wa sukari sokoni mpaka pale viwanda vya ndani vitakapoanza uzalishaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live