Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sita wahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa makosa ya kuua

Hukumu Pc Data Sita wahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa makosa ya kuua

Sun, 2 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu sita wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa na Mahakama Kuu ya Tanzania kwa makosa ya kuua watu wawili katika matukio mawili tofauti yaliyotokea Igunga, mkoani Tabora na Songea mkoani Ruvuma.

Katika tukio la kwanza, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imewahukumu kunyongwa hadi kufa watu watano ambao ni wakazi wa Igunga baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya kumuua mume wa mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi (albino), alipokuwa akijaribu kumwokoa mke wake asikatwe mkono.

Tukio jingine limetokea Wilaya ya Songea ambapo Mahakama Kuu Kanda ya Ruvuma, imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa mtu mmoja aliyekutwa na hatia ya kumuua mwalimu mmoja wilayani humo.

Katika tukio la Tabora, watu watano walidaiwa kumuua mume wa mwanamke mmoja mwenye ualbino wakati akijaribu kumwokoa mke wake asikatwe mkono kwa imani za kishirikina.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, aliyekasimiwa mamlaka ya ziada, Jovin Katto baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Katika hukumu hiyo, Katto alisema upande wa mashtaka umethibitisha pasipo shaka washitakiwa hao walitenda kosa hilo la kinyama ambalo adhabu yake ni moja ya kunyongwa hadi kufa.

Waliopewa adhabu hiyo ni Mussa Masanilo, Mhoja Shija, Regina Kashinje, Elizabeth Masanja Shija na Biria Masanja.

Katto, ambaye ni miongoni mwa mahakimu walioongezewa mamlaka ya kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu, alisema washitakiwa baada ya kumshambulia Mapambano Mashiri kwa mapanga hadi kufa, walimkata mkono wa mke wake huyo mwenye ualbino.

Awali, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili Merito Ukongoj, uliiambia Mahakama hiyo kwamba washtakiwa walitenda kosa hilo Agosti 16, 2014 usiku katika kijiji cha Buhekela, wilayani Igunga.

Alisema siku hiyo saa nne usiku, washtakiwa walivamia nyumbani kwa Mashiri ambaye kwa sasa ni marehemu na kumkatakata kwa panga hadi kusababisha kifo chake. Katika shauri hilo, Katto alimhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitano jela, Bahati Kulugu ambaye alikutwa na mkono wa mama huyo.

Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kwamba Bahati Kalugu alikamatwa akiwa na mkono huo wa mwenye ualbino akitafuta mnunuzi.

Huko Songea, Mahakama Kuu Kanda ya Songea imemhukumu kunyongwa hadi kufa, mkulima mmoja wilayani humo, Orestus Mbawala (51) ambaye ni maarufu kwa jina la Bonge.

Hukumu hiyo ilitolewa Septemba 28 mwaka huu na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Yose Mlyambina baada ya kupitia hukumu hiyo na kuridhishwa na ushaidi uliotolewa Mahakamani hapo.

Katika kesi hiyo, Mbawala na mshtakiwa mwenzake aitwaye Cosmas Mbena walituhumiwa kumuua Christopher Ndimbo aliyekuwa mwalimu wa shule ya Lupapila.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live