Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sita wadakwa na bunduki ya AK 47, risasi 31

15605 Moro+pic TanzaniaWeb

Wed, 5 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro.  Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu sita  kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya AK47 ikiwa na risasi 31.

Mbali na risasi hizo zilizokuwa katika magazine mbili, watu hao pia wamekutwa na vifaa vya kuvunjia mageti, pesa taslimu Sh67,700 pamoja vitu vingine vinavyodhaniwa kuwa ni vya wizi.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 4, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema  watuhumiwa hao walikamatwa jana  jioni eneo la Kihonda.

Kamanda Mutafungwa amesema watuhumiwa hao ambao majina yao  yamehifadhiwa kwa sasa kwa sababu za uchunguzi, walikamatwa kufuatia tukio la unyang’anyi kwa kutumia silaha walilolifanya Agosti 26, 2018.

Amesema katika tukio hilo watuhumiwa hao walimvamia mfanyabiashara wa duka na kumpiga risasi katika mguu wa kushoto kisha kumpora Sh7.1milioni.

Katika tukio jingine, Mutafungwa amesema wahamiaji haramu kutoka nchini Ethiopia walikamatwa katika  kijiji cha Maseyu- Mikese wakiwa wamejificha vichakani baada ya dereva wa gari lililowabeba kuwashusha na kuwatelekeza.

Kamanda Mutafungwa amesema polisi kwa kushirikiana na idara ya uhamiaji inaendelea kuwahoji wahamiaji hao ili hatua zaidi zichukuliwe dhidi yao.

Wakati huo huo polisi mkoani Morogoro imemkamata Rajabu Severine akiwa na magunia 12 ya bangi yenye uzito wa kilogramu 180 pamoja na mbegu za bangi kilo 30 iliyokuwa imehifadhiwa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.

Amesema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz