Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sita mbaroni wakidai pesa zao za DECI

49875 Pic+deci

Tue, 2 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu sita wanaodai kuwa walikuwa wanachama wa kampuni ya mchezo wa upatu ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), wametiwa mbaroni.

Watu hao wametiwa mbaroni leo Jumatatu, April Mosi, 2019 baada ya kujitokeza Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kudai fedha zao walizokuwa wameziwekeza DECI, kabla ya viongozi wa kampuni hiyo kukamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kuendesha shughuli hizo za upatu.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Mashitaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga, alifungua maombi mahakamani hapo akiomba amri ya mahakama kutaifisha mali za kampuni hiyo zikiwemo fedha kiasi cha Sh14.1 bilioni zilizokamatwa na kuzuiliwa kufuatia kesi hiyo, nyumba, viwanja vinane pamoja na magari ya kifahari 11.

DPP amewasilisha maombi hayo dhidi ya waliokuwa viongozi wa DECI, Jackson Sifael Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saiguran Ole Loitg’nye na Samwel Sifael Mtares.

Viongozi hao wa DECI walikamatwa na kushtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Juni 2009, kwa kosa la kujihusisha na shughuli hizo za upatu isivyo halali, huku fedha walizokutwa nazo zikishikiliwa na Serikali.

Mahakama hiyo katika hukumu yake Agosti 2013 iliwatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya jumla ya Sh21 milioni, ambapo walilipa faini hiyo na kuepuka kifungo.

Miaka sita baadaye baada ya hukumu hiyo, ndipo DPP akawasilisha maombi hayo ya kutaifisha mali zao.

Siku chache baada ya DPP kuwasilisha maombi hayo, limeibuka kundi lingine la watu 18 ambao nao wamewasilisha maombi ya kujumuishwa katika maombi hayo ya DPP, dhidi ya viongozi hao wa DECI, wakidai kuwa walikuwa miongoni mwa wanachama waliopanda mbegu zao DECI na hivyo wanaomba wapewe pesa zao.

Maombi hayo ya DPP pamoja na wanachama hao wa zamani wa DECI yalikuwa yamepangwa kusikilizwa leo Jumatatu na Jaji Stephen Magoiga, lakini Jaji Magoiga akaahirisha usikilizaji huo hadi kesho asubuhi, akieleza kuwa alikuwa na dharura na akaamuru waombaji wa pande zote na hao wapandaji 18 wafike mahakamani kesho asubuhi kwa ajili ya usikilizwaji wa maombi hayo  yote.

Hata hivyo baada ya kutoka tu ndani ya ukumbi wa mahakama, wapanda mbegu hao wakatiwa mbaroni na polisi na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Waliotiwa mbaroni ambao ndio waliofika mahakamani kati ya waombaji wote 18 ni  Andrew Tungaraza, Frida Msuva, Imelda Adolph, Jackson Nyera, Tadea Mgoso na Philemon Mwarko.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz