Dar es salaam. Wafanyabiashara watano na dereva mmoja, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Tanzania wakikabiliwa na shtaka moja la usafirishaji wa bangi.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Alhamis Septemba 4, 2019 na kusomewa shtaka hilo na wakili wa Serikali, Tuli Helela .
Washtakiwa hao ni Shabani Salum Juma mkazi wa Gongo la Mboto, Yahaya Majaba mkazi wa Ukonga Madafu na Ezekiel Patrick maarufu Dudu mkazi wa Gongo la Mboto Ulongoni A.
Wengine ni Abdul Rabi Abdulrahahim maarufu Nkupe na mkazi wa Gongo la Mboto Ulongoni B na Ginziari Aidan mkazi wa Kiwalani Migombani na Mnyamani Juma (30) mkazi wa Tabata Relini Dar es Salaam.
Akiwasomea shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Vicky Mwaikambo, Wakili Helela amedai kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya bangi.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 16, 2016 eneo la njia panda ya Segerea wilayani Ilala.
Pia Soma
- Wanawake kuwekewa mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara mipakani
- Kesi ya wanafunzi wa KIU kumdhihaki Rais Magufuli kuendelea Oktoba 8
- Kesi ya dhahabu: Washatakiwa wahukumiwa kulipa faini Sh230 milioni au kwenda jela miaka 15
Hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Hakimu Mwaikambo aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 19, 2019 itakapotajwa tena na washtakiwa wamerudishwa rumande .