Dar es Salaam. Watu sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kukutwa na vipande 413 vya meno ya tembo na viwili vya meno ya kiboko, yote yakiwa na thamani ya Sh4.03 bilioni.
Washtakiwa hao ni Hassani Likwena (39), Bushiri Likwena, Oliver Mchuwa (35), Salama Mshamu (21), Haidary Sharifu (44) na Joyce Thomas (33).
Akizungumza leo Jumanne Septemba 17, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon amesema washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kushiriki genge la uhalifu, kukutwa na vipande vya meno ya tembo na kiboko pamoja na kutakatisha fedha.
Simon amedai kati ya Januari Mosi, 2017 na Septemba 3, 2019 maeneo tofauti Mkoa wa Mtwara , Pwani na Dar es Salaam washtakiwa walishiriki genge la uhalifu kwa kupokea nyara za Serikali; vipande 413 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola 1,755,000 za Marekani na vipande viwili vya meno ya kiboko vyenye thamani ya Dola 1500 za Marekani.
Katika shtaka la pili, Septemba 3, 2019 maeneo ya Saku Chamanzi jijini Dar es Salaam, kwa pamoja walikutwa na nyara za Serikali ambazo ni meno hayo ya tembo bila ya kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.
Simon amedai shtaka la tatu Septemba 3, 2019 maeneo ya Saku Chamanzi walikutwa vipande viwili vya meno ya kiboko kinyume na sheria mali ya Serikali bila ya kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.
Pia Soma
- Watu 24 wauawa katika shambulio la kujitoa muhanga
- Kituo cha afya Daraja Mbili Arusha sasa kufanya upasuaji
- MWANANCHI JUKWAALA FIKRA: Mbinu hizi zitawawezesha wahitimu kujiajiri wenyewe
- Wanne wahukumiwa kunyongwa hadi kufa
Baada ya maelezo hayo wakili Simon amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, kuomba tarehe kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mwaikambo amesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kuahirisha kesi hadi Oktoba Mosi, 2019.