Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sirro awaonya wanaojipanga kufanya uhalifu

Sirrropic Data Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro

Sun, 12 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amewaonya wanaojipanga kufanya uhalifu wa kutumia silaha katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kigezo cha kutafuta fedha.

Akizungumza leo Jumapili Desemba 12, 2021 wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya askari wa jeshi hilo, Sirro amesema wapo macho, “tunapokaribia sikukuu za mwisho wa mwaka wale ambao silaha zao wamezifisha wanaamua kuingia barabarani kutafuta fedha.”

“Sasa niwaombe sana Watanzania tumalize mwaka vizuri. Huna sababu ya kuingia kwenye makosa haya ya bunduki unatisha Watanzania bila sababu na kujiweka maisha yako hatarini.”

Kuhusu usalama nchini,  amesema hali ni shwari ingawa bado  kuna matukio ya uhalifu huku akikiri kuwepo kwa changamoto ya uhalifu wa  makosa yanayovuka mipaka ni yale yanayoashiria ugaidi, usafirishaji dawa za kulevya na binadamu.

Sirro amesema wameweka mikakati kadhaa ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi, kushirikisha viongozi wa vijiji, mitaa, kata na shehia katika doria za mitaani na kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.

Mikakati mingine ni kufanya doria za kawaida na doria maalum kuwasaka wahalifu na kuwashughulikia pamoja na kupunguza ucheleweshaji wa upelelezi ambako  kesi kubwa  upelelezi wake hautakiwi kuzidi mwaka na kesi ndogo miezi sita.

Advertisement

Akizungumzia askari walipanda daraja la uofisa amesema, “hawa ni wasomi tunaamini utendaji utakuwa mkubwa, tunategemea utendaji kazi utabadilika kwa sababu ya usomi wao. Ni imani yangu maofisa hawa watatoa mchango chanya kwa Taifa kulingana na hali ya sasa ya sayansi na teknolojia.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live