Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sintofahamu yatawala kifo cha kijana Kigamboni

74329 Kifo+pic

Thu, 5 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakuna kitu kinauma kama mzazi kumpoteza mtoto wake tena kupitia sehemu aliyokuwa akidhani ni salama.

Hali hiyo imemkuta Edna Clement, mama wa watoto wanne ambaye kwa sasa yupo katika kipindi kigumu cha kumpoteza mwanaye wa kwanza, Innocent Vitus kutokana na kile kinachodaiwa alishambuliwa na wananchi wenye hasira.

Edna na watoto wake wanaishi eneo la Kibugumo, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

“Ilikuwa Alhamisi saa 2:00 usiku nilisikia kijana wangu wa pili akaniita mama kaka kakamatwa na polisi, nilikimbia hadi kwenye lile gari na kuwauliza wanakompeleka mwanangu usiku wakaniambia mwanangu hayumo,” alisimulia Edna na kuongeza: “Nikamuuliza mdogo wake mbona simuoni akasema mama yupo huwezi kuona vioo ni vyeusi basi gari ikaondoka, kwa mbele kidogo ili igeuze nikasimama katikati ya barabara nikawaambia sitoki hadi mniambie mnakompeleka, wakasema kituo cha polisi.”

Alisema wakati ya gari linaondoka aliwasiliana na baadhi ya ndugu zake waliomsihi kutulia ili wafuatilie.

Hata hivyo, Edna alisema usiku huohuo aliamua kwenda kituo cha polisi na saa 4:00 usiku alishuhudia kijana wake akiingizwa mahabusu ya kituoni hapo.

Pia Soma

Advertisement
Alisema alirudi nyumbani na Agosti 30 saa 4:00 asubuhi alimpelekea chai lakini alishangaa kusikia kuwa hawezi kutembea. “Alipoitwa mmoja wa mahabusu aliniambia ‘mama huyu kaumia mguu hawezi kutembea’, hivyo akaingiza chai na kumpatia, niliomba RB nijue ni nani aliyemkamata na kosa lake,” alisema.

Alisema aliandikiwa jina la mpelelezi alipoingia ofisini kwake alimuuliza jina la mtuhumiwa, lakini alimwambia hana taarifa zake wala hajakabidhiwa jalada la kesi hiyo.

Alisema Agosti 31, alipeleka tena chai lakini kijana wake alipoitwa na askari wa zamu hakuiti, jambo hilo lilimfanya na yeye (Edna) kuanza kuita bila mafanikio huku mahabusu mmoja akijibu tena kuwa alitolewa tangu Alhamisi saa 10:00 jioni na hakurudishwa.

Alisema aliombe namba ya mpelelezi alipompigia alimweleza kuwa kesi ngumu hawezi kuisimamia kwa sababu haina jalada na kwamba, baada ya kufuatilia walimwambia walimtoa mahabusu akataka kukimbia.

Polisi watupiana mpira

Septemba 2, gazeti hili lilimtafuta kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuthibitisha tukio hilo lakini alijibu: “Nipo likizo wasiliana na mtu niliyemuachia madaraka.”

Baada ya kuwasiliana na ofisi ya Mambosasa, walimwelekeza mwandishi kuwasiliana na kamanda wa polisi mkoa wa Temeke ambaye naye alidai hana taarifa hizo. “Naomba niwatafute eneo husika ambao ni Kigamboni niweze...uwe mvumilivu na kesho unipigie,” alisema Amon Kakwale ambaye ni kamanda wa polisi Temeke.

Septemba 3, simu yake ilipopigwa ilipokewa na msaidizi wake ambaye alidai kamanda yuko kikaoni huku akimtumia mwandishi namba ya simu ya mkuu wa kituo cha polisi Kigamboni kurahisisha upatikanaji taarifa. Hata hivyo, mkuu huyo wa kituo alisema: “Anayeweza kuzungumzia hayo ni RPC Temeke naomba umtafute kwa sababu ndiyo nasikia kutoka kwako, wasiliana naye ila mimi kwa kweli sijui.”

DC akataa kuzungumzia

Mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri alipopigiwa simu alisema msibani mkoani Mwanza. “Mambo ya kesi nendeni kwa OCD niko msibani Mwanza,” alisema Sarah.

Mazishi utata

Awali, Edna alikataa kuzika mwili wa kijana wake hadi atakapojua sababu za kifo na kukamatwa kwake. Hata hivyo, mjomba wa marehemu Jackson Vincent alisema wameamua kuzika kwa sababu waliambiwa kufanya hivyo na polisi waliowasindikiza kufanya uchunguzi.

“Tulikuwa na askari sita tulipoenda kufanya uchunguzi, tulipofika hata daktari mwenyewe hakupata nafasi ya kufanyia uchunguzi ule mwili bali askari ndiyo walitoa maelezo ya kuwa ni jambazi aliuawa akijaribu kukimbia mikononi mwa polisi, maneno hayo yalifanya tuanze kulumbana na wao kunipa kibali cha kuzika kwa lazima na kuambiwa fanyeni mazishi,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz