Njombe. Wakati giza likiwa bado limetanda kwa wananchi wa Wilaya ya Njombe kutokana na matukio ya mauaji ya watoto, Josephina Kihombo, mkazi wa Kijiji cha Ikando wilayani hapa ameiangukia Serikali akiitaka imsaidie kumpata mwanaye, Gaudence Kihombo (7) ambaye hajulikani aliko tangu atoweke nyumbani Januari 6.
Tukio la kupotea kwa mtoto huyo linahusishwa na matukio ya utekaji na kuuawa kwa watoto ambapo hadi sasa watoto 11 wameuawa kwa kuchinjwa na mmoja alinusurika kupelekwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu.
Jana, Mwananchi lilifika nyumbani kwa mama huyo na kufanya naye mahojiano ambapo aliiomba Serikali imsaidie ili mwanaye aweze kupatikana.
“Mwanangu amepotea Jumapili ya Januari 6, wananchi walijitokeza porini kumtafuta lakini baada ya hapo tukaambiwa sisi ndugu ndio tuendelee wenyewe kumtafuta,” alisema Josephina.
Alisema suala hilo liliendelea kuwa kimya hadi yalipotokea mauaji ya watoto watatu wa familia moja kijijini hapo na uongozi wa Mkoa wa Njombe ulipofika ndipo akatoa malalamiko ya kupotea kwa mwanaye. “Ninaamini kama suala la mtoto wangu lingetiliwa mkazo na vyombo vya dola, hata haya mauaji ya watoto watatu pengine yasingetokea maana hawa watoto watatu walitekwa tarehe 20, wakati mwanangu alipotea tarehe 6.”
Rehema Kipagate, bibi wa mtoto huyo alisema mazingira ya kutoweka kwa mjukuu wake anayesoma darasa la pili Shule ya Msingi Ikando yanashangaza.
Alisema Jumapili ya Januari 6, alimwacha mjukuu wake huyo nyumbani na kwenda kanisani, lakini aliporudi mchana hakumkuta.
Alisema kwa vile siyo kawaida mjukuu wake huyo kuondoka nyumbani peke yake, aliingiwa na hofu, hivyo aliwauliza majirani ambao walimwambia kwamba alionekana na watoto wenzake wawili wakielekea kuchunga ng’ombe. “Niliambiwa kuna wenzake wawili waliokuwa wanakwenda kuchunga ng’ombe porini ndio wamemchukua, nikakaa hadi jioni hakuonekana,” alisema.
Alisema ilipofika saa 4 usiku alizidi kuingiwa na hofu na asubuhi aliulizia tena kwa majirani, lakini jibu lilibaki lilelile.
Hata hivyo, alisema baadaye alifuatwa na kijana mmoja (hakumtaja jina) aliyemwambia Gaudence alimfuata kanisani.
“Lakini nilipomfuata tena kumuuliza vizuri nikagundua alikuwa ananidanganya, na alikiri kwamba kweli walikuwa wote wakichunga ng’ombe wao na alimuacha kwenye machungio, ndipo nikatoa taarifa serikali ya kijiji kuhusu kupotea kwa mjukuu wangu.”
Alisema baada ya viongozi wa kijiji kumbana kijana huyo aliwaonyesha maeneo matatu waliyokwenda kuchunga porini, lakini sehemu ya tatu aliyoonyesha alisema ndipo walimwacha hapo na yeye na wenzake wakaenda kuchuma matunda, lakini waliporudi hawakumkuta.
Alisema ilipofika siku ya tatu, uongozi wa kijiji ulimwamuru Rehema atoe taarifa polisi mjini Makambako, huku wakiwaambia ndugu waendelee kumtafuta.
“Nilisema polisi siwezi kwenda peke yangu, hapa ni lazima tuwe na wale vijana waliokuwa na mjukuu wangu, ndipo siku ya nne nikaandikiwa barua na serikali ya kijiji nikaenda mwenyewe kutoa taarifa.”
Uongozi wa kijiji
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikando, Melkion Kaduma alisena taarifa za kutoweka kwa mtoto Gaudence walizipata na walishiriki kumsaka, lakini hadi sasa hajapatikana.
“Kweli ndugu wale walitoa taarifa siku mbili tangu kupotea kwa mtoto yule, hapo tukapiga ngoma kijiji kizima na vijiji jirani na kuanza kusambaa porini na kando kando mwa mito kumtafuta bila mafanikio,” alisema Kaduma.