Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi askari JKT aliyemchinja mzazi wake

Mnhhyyggbnm Simulizi askari JKT aliyemchinja mzazi wake

Sun, 16 Jan 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

“Nimemaliza kuchinja kuku”. Ni maneno ya mashuhuda wakielezea kauli ya Mussa Edward anayedaiwa kumuua kikatili baba yake mzazi, Edward Ndonde aliyemchinja kwa kutumia kisu.

Ndonde aliyewahi kuwa mwalimu, aliwahi pia kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM kabla ya kustaafu.

Tukio hilo lilitokea Jumatano Januari 12 mwaka huu katika mtaa wa Lumbira Kata ya Iwambi jijini Mbeya, likiwaacha ndugu na majirani wakiduwaa na kushikwa na simanzi.

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya mashuhuda walisema mauaji hayo hayakuchukua muda mrefu na walipokuja kuona walikuta damu zimetapakaa ndani na mtu ameshafariki.

Alex Mwang’ande ambaye ni jirani kwa marehemu, alisema alishtushwa na taarifa hizo, kwani kabla ya tukio hakufahamu mapema kilichokuwa kinaendelea hadi aliposikia kelele zikitoka ndani ya nyumba marehemu.

Advertisement Alisema baada ya kelele hizo, alifika nyumbani kuona kinachoendelea ambapo mtuhumiwa aliweza kumpokea akimwambia amemaliza kuchinja kuku sebuleni, hali iliyompa wasiwasi kwa kauli hiyo.

“Baada ya kuingia ndani mama yake na mtuhumiwa akawa analia kwa uchungu, huku mtuhumiwa akisema amemaliza kuchinja kuku, tunakuja kuangalia vizuri tukakuta damu zimemtapakaa sehemu za mikononi hadi mwilini”

“Hapo nilikuwa na balozi wa mtaa, tukaamua kuingia ndani kuona huyo kuku aliyechinjwa tukakuta tayari ni baba yake ameshakufa tayari akiwa majeraha kutokana na kuchomwa kisu ambacho kilikuwa kimevunjika kimetupwa pembeni” anasema Mwang’ande.

Aliongeza kuwa mbali na tukio hilo, mtuhumiwa na baba yake walikuwa na ugomvi wa muda mrefu kwani ni zaidi ya mara moja amewahi kuamua ugomvi wao kwa vipindi tofauti.

Aliongeza kuwa baada ya wananchi kuona unyama huo, walimvaa mtuhumiwa na kuanza kumpa kichapo, ambapo aliingilia kati na kuita Jeshi la Polisi ambalo liliweza kumchukua.

Naye Misijinari Hashim alisema ni masikitiko makubwa kumpoteza jirani yao kwa kifo kibaya kwa kuuawa na mwanawe na kwamba hawawezi kumsahau kwa wema aliofanya mtaani hapo.

“Ni masikitiko makubwa sana, tukio limetuacha na mshtuko na simanzi kubwa sisi majirani zake, tutaendelea kumkumbuka kwa mazuri” alisema Misijinari.

Kwa upande wake, Balozi wa Mtaa huo, Hezron Thobias anasema tukio hilo lilitokea majira ya saa 4 asubuhi, akiwa anatoka kwenye shughuli zake alikuta taarifa mtaani kwake wakimueleza kilichotokea kwa marehemu.

Alisema katika kumchunguza mtuhumiwa walibaini alikuwa ameweka ugoro mdomoni akionekana kuwa amelewa, huku akieleza kuwa wawili hao hawakuwa na maelewano mazuri kwa kipindi cha nyuma.

Alisema enzi za uhai wake marehemu alikuwa kiongozi mwenye busara na alikuwa akitumiwa kutoa ushauri kwa viongozi wakiwamo wa chama chake cha CCM.

“Marehemu alikuwa mtu wa busara ambaye alipenda ushirikiano, mchapakazi na mwenye maadili, ni pigo kubwa mtaani kwetu” alisema Thobias.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Alhaji Saad Kusilawe alisema marehemu alikuwa mtumishi mwenzao kwenye chama kabla ya kustaafu.

Anasema katika uhai wake aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wazazi Taifa hadi anastaafu na alikuwa mwadilifu katika utumishi wake na alikuwa kama hazina katika kutoa ushauri kwa vijana wanaochipukia.

“Ni mshtuko na pigo kubwa kwani ameacha pengo na ni masikitiko kwani alikuwa mashuhuri na tulihitaji zaidi busara zake, lakini tunakubaliana na kilichotokea na nitoe pole kwa ndugu, jamaa na ndugu na chama kwa ujumla” alisema Kusilawe.

Mwanasikolojia

Mtaalamu wa saikolojia, Flora Magabe anasema vitendo vya mauaji vimekithiri sana, akibainisha kuwa kwa uzoefu huwa mara nyingi vinasababishwa na upungufu wa akili, imani, mila na tamaa za maisha.

“Kwa kipindi kifupi yameripotiwa matukio mengi ya mauaji, jamii ielimishwe, kwa sababu mambo mengine ni kutokana na imani, mila na tamaa za maisha” alisema Flora.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz