Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simu tatu zakabidhiwa mahakamani kwa ushahidi

52896 Pic+simu

Thu, 18 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Hashim Ally, shahidi wa 17 upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Sekondari ya Scolastica, Humphrey Makundi, amekabidhi simu mbili za mshtakiwa wa tatu, Laban Nabiswa katika Mahakama Kuu.

Mbali na simu hizo kupokewa, tayari mahakama ilishapokea nyaraka mbalimbali za mawasiliano kutoka kampuni ya Vodacom zilizoonyesha muda wa maongezi katika simu za washtakiwa hao kuanzia siku ya tukio la mauaji kati ya Novemba 6 hadi 20, 2017.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Firmin Matogolo huku akiongozwa na wakili wa mashtaka Omari Kibwana, Ally aliiambia mahakama hiyo kuwa Novemba 17, 2017 saa 4:00 usiku alipokea maelekezo kutoka kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa (RCO) mkoani Kilimanjaro, kupokea vielelezo kutoka kwa Afande Tenga, ambapo miongoni mwa vielelezo hivyo zilikuwa simu mbili za mshtakiwa huyo.

Shahidi huyo ambaye alikuwa ni mtunza vielelezo katika ofisi ya RCO aliieleza mahakama hiyo kuwa simu hizo za mshatakiwa wa tatu zilikua na laini tatu ambapo simu moja aina ya Samsung ilikuwa na laini mbili na simu moja ya Itel ilikua na laini moja.

Aidha shahidi huyo alidai Novemba 17, 2017 wakati akichukua maelezo ya mshtakiwa wa kwanza Hamis Chacha katika chumba cha upelelezi alikiri kutenda kosa la mauaji ya mwanafunzi huyo na alisema alishirikiana na Laban Nabiswa ambaye alikuwa mwalimu wa nidhamu na Edward Shayo ambaye ni mmiliki wa shule hiyo.

Katika kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia inadaiwa kuwa Novemba 6, 2017 Humphrey aliuawa kisha mwili wake kuokotwa mto Ghona takriban mita 300 kutoka eneo la shule hiyo.

Related Content

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa na wakili mkuu wa Serikali Joseph Pande akisaidiwa na mawakili waandamizi Abdallah Chavula, Omari Kibwana na Lucy Kyusa huku ule wa utetezi ukiongozwa na Elikunda Kipoko, Wakisa Sambo, Patrick Paul na David Shilatu.

Sehemu ya mahojiano na shahidi huyo na wakili wa upande wa utetezi yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Shilatu: Ni kweli kwamba kielelezo kinavyotoka kwa muda mfupi lazima taarifa ziingizwe kwenye fomu namba 16?

Shahidi:Ni sahihi

Wakili Shilatu: Ni kweli kwamba fomu namba 16 hujaileta hapa mahakamani.

Shahidi: Mimi sijaileta

Wakili Shilatu: Wewe ulihusika katika kumkamata Hamis Chacha na wenzake?

Shahidi: Sikumkamata

Wakili Shilatu: Ni kweli wewe na wenzako mlimpiga sana Chacha?

Shahidi:Hayo ni ya kwako. Nilikuwa tu mimi na yeye wakati nikichukua maelezo yake.

Wakili Shilatu: Ni kweli Chacha alikuambia amepigwa?

Shahidi:Hayo unasema wewe.

Wakili Shilatu: Umeiambia mahakama ulianza mahojiano na Hamis Chacha saa 5:23 usiku?

Shahidi: Ni Kweli

Wakili Shilatu: Ulitegemea saa tano usiku awapate wapi ndugu zake kutoka Mara?

Shahidi: Siyo wajibu wangu

Wakili Shilatu: Ulikuwa na haraka gani ya kuchukua maelezo kuanzia saa 5:23 hadi kesho yake saa 8:40?

Shahidi: Ni masaa tu.

Wakili Shilatu: Ni wakati gani Hamis Chacha alinyang’anywa simu?

Shahidi: Sijui

Wakili Shilatu: Ni kweli kwamba Hamis Chacha alikuambia amepigwa na polisi?

Shahidi: Hayo unazungumza wewe.

Wakili Shilatu: Wewe ulimuona Hamisi Chacha akimuua huyo mwanafunzi uliyemtaja kwa majina?

Shahidi: Sikumuona

Wakili Shilatu: Wewe ulimuona mshtakiwa wa pili na mwingine wakimuua mwanafunzi?

Shahidi: Sikuwepo eneo la tukio. Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake Jaji Matogolo aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 29, mwaka huu kwa kile alichosema kuwa muda aliopangiwa kuisikiliza umekwisha.

“Muda niliopangiwa kusikiliza kesi hii umeisha, hivyo naahirisha kesi hii mpaka Aprili 29 mwaka huu,” alisema Jaji Matogolo.



Chanzo: mwananchi.co.tz