Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Silaha 160 za uhalifu, ujangili zakamatwa

3df254065f58b6158cb2303a6cfd6b0e.png Silaha 160 za uhalifu, ujangili zakamatwa

Wed, 10 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JESHI la Polisi Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Kikosi cha Kudhibiti Ujangili cha Pori la Akiba Liparamba chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Kusini limekamata silaha 160 za aina mbalimbali zilizokuwa zikitumika katika matukio ya uhalifu ikiwamo ujangili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Marwa amesema mbali na silaha hizo, pia wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 68 waliokutwa wakifanya matukio ya ujangili kwenye hifadhi na wengine wakimiliki silaha kinyume cha sheria.

Alisema kukamatwa kwa silaha hizo kumetokana na msako mkali wa silaha haramu na watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na ujangili unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.

Kamanda Maigwa ametaja silaha hizo ni magobole 149, rifle tatu na shortgun nane ambazo alisema kama zingeendelea kuwapo mikononi mwa wahalifu zingesababisha madhara mbalimbali ikiwamo kuua wanyamapori na kufanya ujambazi na makosa mengine yanayohusiana na matumizi ya silaha.

Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, silaha hizo zitateketezwa kwa kufuata taratibu za kisheria za ili zisilete madhara na zilizokutwa na watuhumiwa zitatumika mahakamani kama sehemu ya vielelezo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kusini, Keneth Sanga alisema wamejipanga vyema kukabiliana na vitendo vyote vya ujangili na majangili kwenye hifadhi na mapori ya akiba na kuwaonya watu kuacha vitendo hivyo kwani vinaweza kuwapeleka mahali pabaya ikiwamo kupoteza maisha.

Chanzo: habarileo.co.tz