Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Sikupata uthibitisho kama Aneth aliingiliwa’ kimwili’

Msuya Dada 0 ‘Sikupata uthibitisho kama Aneth aliingiliwa’ kimwili’

Wed, 30 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Shahidi wa 21 katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya, Dk Hassan Mwinchande wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ameieleza Mahakama kuwa hakupata ushahidi kama marehemu aliingiliwa kimwili kabla ya kifo.

Kwa upande wake, shahidi wa 22, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, David Mhanaya aliieleza mahakama kuwa alimhoji aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa marehemu Aneth, aliyemweleza namna watu wawili walivyofika nyumbani kwake na kumuahidi kumpatia Sh50 milioni kama atafanikisha kazi maalumu.

Mashahidi hao walieleza hayo jana wakati wakitoa ushahidi wao mahakamani hapo, kwa nyakati tofauti kwenye kesi hiyo inayoendelea kusikilizwa.

Aneth alikuwa mdogo wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro Agosti 7, 2013. Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke na mwili wake kukutwa ndani ya nyumba yake ukiwa mtupu, huku nguo yake ya ndani ikiwa pembeni yake.

Kutokana na hali hiyo, Polisi walihisi Aneth kabla ya kuuawa, alikuwa ameingiliwa kimwili kwa nguvu.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 103/2018 inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ni Miriam Steven Mrita, ambaye ni mjane wa Bilionea Msuya na mwenzake, Revocatus Muyalla.

Katika ushahidi wake jana akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Yasinta Peter shahidi huyo (Dk Chande), alisema ndiye aliyefanya uchunguzi wa mwili wa Aneth, Mei 26, 2016 ili kujua sababu za kifo.

Baada ya kumaliza alikabidhi mwili wa Aneth kwa ndugu na askari na baadaye aliandika ripoti kisha akasubiria vipimo vingine ambavyo sampuli zake zilichukuliwa kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kutokana na uchunguzi huo, alibaini Aneth alivuja damu nyingi, hali iliyosababishwa na kuvunjika shingo na koromeo.

Alidai kuwa alibaini pia mwili ulikuwa na jeraha shingoni kwa mbele lenye ukubwa wa sm10 na viganja vya mikono vilikuwa na matone ya damu.

Ingawa uchunguzi ulifanyika Mei 26, 2016 lakini ripoti ya uchunguzi huo ilijazwa Juni 14, 2016 kwa sababu kuna vinyama na mpanguso wa sehemu za siri za marehemu vilivyochukuliwa kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi, ndivyo vilikuwa vikisubiriwa kwa kuwa majibu yalichukua muda kutoka.

Lengo la uchunguzi huo lilikuwa kuthibitisha matokeo ya mwonekano wa macho kujua kama jeraha lilitokea kabla au baada ya kifo.Baada ya uchunguzi ilibainika kuwa lilikatwa wakati bado marehemu akiwa hai.

Wakati akihojiwa na mawakili wa utetezi, Peter Kibatala na Nehemiah Nkoko, shahidi huyo alijibu kuwa hakukuwa na uthibitisho kama Aneth aliingiliwa kwa kuwa hakukuwa na mbegu za kiume ndani ya sehemu zake za siri.

Hata hivyo, akifafanua zaidi alikana kusema marehemu hakubakwa huku akifafanua kuwa kubaka ni mpaka anayemuingilia mwanamke awe amemwaga mbegu za kiume.

Sehemu ya mahojiano baina yao ilikuwa kama ifuatavyo;

Kibatala: Hii Police form namba 99 ndio reguesting form? (Fomu ya maombi ya uchunguzi)

Shahidi: Ndio ‘reguesting form’

Kibatala: Anampatia shahidi nyaraka fulani kisha anamuuliza kama anaitambua

Kibatala: Hiyo fomu unaitambua?

Shahidi: Naitambua

Kibatala: Ni nini?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji daktari anapofanya uchunguzi huchukua vitu vingi, ikiwamo vinyama vya shingoni na vitu vya ndani na kupeleka kwa mkemia Ili kujiridhisha kama hakupewa sumu.

Jaji: Hiyo fomu inaitwaje?

Shahidi: Ndio nakuja huko Mheshimiwa Jaji katika kufanya uchunguzi unapaswa…

Kibatala: Shahidi bila kuonekana kuwa nakuletea usumbufu hiyo fomu inaitwaje? kwani kuna ugumu gani kusoma kama ilivyoandikwa kuwa investigation form (fomu ya uchunguzi)?

Shahidi: Ndio nilikuwa nafanya, hii inaitwa investigation form (fomu ya uchunguzi).

Kibatala: Kwenye hii fomu una majibu ya request (maombi) ya uchunguzi wa sampuli zilizopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali uliyofanya?

Shahidi: Sina

Kibatala: Lakini ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali walirudisha kwako?

Shahidi: Bado sijayaona mpaka sasa

Kibatala: Na bado mnataka Mahakama hii iamini kuwa marehemu hakufa kwa sumu.....Kwenye hii fomu kuna item imeandikwa chemical investigation, ni kweli kwamba hii iliwekwa mahsusi ili kupata matokeo ya kwa mkemia na ulipaswa kujaza?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Ulijaza hujajaza?

Shahidi: Sikujaza kwa sababu.

Maneno hayako hivyo, mimi siko hapa kusema yes or no (ndio au Hapana)

Kibatala: Shahidi, kila mahali kuna masharti yake sio kama ofisini kwako.

Jaji: Muache shahidi ajibu

Shahidi: Sikujaza kwa sababu haikuja kwangu.

Kibatala: Katika kesi hii pia damu ni jambo la muhimu sana, ulisema viganja vya marehemu vilikuwa na damu, unafahamu damu iliyokuwa kwenye viganja vya marehemu ni ya nani?

Shahidi: Sijui

Kibatala: Pengine tungepima tungeweza kujua kama ilikuwa ni ya muuaji au ya marehemu mwenyewe?

Shahidi: Ndio

Nehemiah Nkoko: Shahidi, kwa mujibu wa ripoti yako kwa kuwa marehemu hakukutwa na mbegu za kiume ni dhahiri hakubakwa?

Shahidi: Kubakwa ni suala lingine

Nkoko: Kwa nini ulikwenda kupima kama marehemu alikuwa nazo?

Shahidi: Nilitaka kujua kama aliingiliwa na mtu akamwaga (mbegu)

Nkoko: Kama ulishafanya uchunguzi ukajua chanzo cha kifo nani alikuomba ukafanye uchunguzi wa kuingiliwa?

Shahidi: Ilikuja fomu ya polisi inanitaka nifanye uchunguzi, kwani uchunguzi wa mwili mzima lazima ukamilike?

Nkoko: Kwa hiyo hukuwa na uhakika kama sababu za kifo cha marehemu ni kutokwa na damu na mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi, ni kweli au si kweli?

Shahidi: Siyo kweli kwa sababu..

Nkoko: Mimi sitaki sababu nimekuliza ni kweli au si kweli?

Shahidi: Hayo maswali ya kweli au si kweli mimi huwa siyapendi.

Jaji: Wewe jibu.

Shahidi: Tunapofanya uchunguzi hatujui sababu za kifo, hivyo tunachunguza kila kitu ili kujiridhisha.

Nkoko: Hii fomu ya maombi uliyoletewa ilikuwa na maelekezo gani uliyopaswa kuchunguza?

Shahidi: Ilikuwa inasema marehemu alikutwa amechinjwa na inasemekana amebakwa.

Nkoko: Ni sahihi kwamba katika maombi ya uchunguzi uliyoletewa ilitakiwa kuchunguza kama marehemu amebakwa?

Shahidi: Si kweli.

Ushahidi wa RCO Arusha

Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri, alisema alikuwa kwenye timu ya upelelezi wa mauaji hayo na kwamba, yeye ndiye aliyemhoji aliyekuwa binti wa kazi wa Aneth, Getruda Mfuru.

Alisema binti huyo alimueleza kuwa alifuatwa na watu wawili mwanamke na mwanaume wakamuulizia nyumbani kwa Aneth naye akawaonyesha na akamwambia na yeye anakaa hapo.

Yule mama akamueleza kuna kazi anataka afanye naye, lakini hakumueleza ni kazi gani, lakini akamueleza angerudi kesho yake na akamtaka yule binti awe msiri asimueleze mtu.

Mei 18, 2016 asubuhi walimfuata tena wakamtaka aingie kwenye gari walilikuwa nalo na ndani akakuta watu wengine watatu wakiwa wameficha sura zao na mmoja akamuwekea bastola begani alipogeuka kutazama, huyo mama akamuuliza anaangalia nini na akamtaka amsikilize yeye.

Hivyo alisikia huyo mama akisema; “Mali nitafute mimi wengine watumie.”

Hivyo huyo mama alimpa simu ndogo aina ya Nokia yenye iliyokuwa na laini ya simu ya Airtel kwa ajili ya mawasiliano kati yao na akamtaka asimuonyeshe mtu kwa sababu wataendelea kumfuatilia.

Kisha walifungua begi wakamuonyesha fedha huku wakimwambia Sh50 milioni ni za kwake kama kazi hiyo ikifanikiwa.

Shahidi alidai Getruda alimweleza baadaye kuwa alimkumbuka mama huyo kwa kuwa aliwahi kumuona Mirerani kwa bibi Msuya alikokuwa akifanya kazi awali na alikuwa ni mke wa Erasto Msuya.

Alidai Mei 23,2016 kati ya saa 8 nchana na 10 jioni, Getruda alipigiwa simu na mama huyo kupitia simu maalumu waliyompatia, akawafuata walikokuwa wamesimama umbali kama mita 200 kutoka nyumba ya marehemu.

Alidai kuwa ndani ya gari alikuwemo mwanamke huyo na yule mwanaume na Getruda alipewa maelekezo maalumu kwamba ikifika tarehe 25 awe ameondoka katika nyumba ya Aneth la sivyo watampitia.

Alidai pia walimuelekeza kuwa simu waliyompatia ahakikishe anaiharibu kabisa ili isionekane na wakampatia Sh20,000.

Mei 25, 2016 asubuhi alipoamka alichukua simu akaificha chini ya kapeti akaondoka na funguo za geti baada ya kulifunga akaelekea kwa mpenzi wake, Sabri Kombo aliyemkuta Feri wakavuka lakini baadaye wakarudi kwa pikipiki kurudisha funguo za geti.

Walipokaribia nyumbani waliona gari la Aneth hivyo binti huyo alimtafuta mwanafunzi akampatia funguo hizo akamuelekeza azipeleke nyumba ya jirani yeye akaondoka na mpenzi wake kuelekea Chanika alikokuwa anaishi.

Kesho yake Mei 26,2016 Getruda alipigiwa simu na ndugu yake anayeitwa Neema ambaye anaishi huko Mererani akamfahamisha kuwa Aneth Msuya amechinjwa kinyama na kwamba na yeye Getruda anatafutwa..

Hivyo Getrude ilimbidi aanze kumuelezea mpenzi wake yote yaliyomtokea ambaye alimshauri aende kutoa taarifa Polisi. Lakini yeye Getruda alimuomba Kombo ampatie nauli na Kombo alimtafuta Sh50,000 akapanda gari akaenda Moshi.Kesi hiyo inaendelea tena leo ambapo shahidi huyo ataendelea na ushahidi wake.

Chanzo: mwanachidigital