Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku ya hukumu kesi ya Tido Mhando kujulikana Novemba 16

24672 Pic+tido TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Novemba 16, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi  itatoa tarehe ya kusomwa kwa hukumu dhidi aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando anayekabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya.

Katika kesi hiyo, Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1milioni.

Hatua hiyo imefikiwa leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumuhoji Tido dhidi ya ushahidi wa utetezi alioutoa mahakamani hapo Septemba 20, 2018.

Leo Tido kupitia mawakili wake Martin Matunda na Dk Ramadhani Maleta waliiarifu mahakama kuwa wamefunga ushahidi wa upande wa utetezi.

Baada ya mawakili hao kueleza hayo, Hakimu Shaidi ameutaka upande wa utetezi na upande wa mashtaka,  Novemba 15, 2018  kuwasilisha hoja za mwisho za  majumuisho ya kesi hiyo.

Akihojiwa na wakili wa Swai,  Tido amedai mchakato mzima wa kuingia ubia wa kuhamisha TBC kutoka katika mfumo wa analojia kwenda Digitali ulifanywa na bodi ya TBC.

Tido amedai kuwa hakuna kitu alichokifanya bila ya ridhaa ya bodi na kwamba  bodi ndiyo ilimuagiza afanye mchakato wa awali na ulipokamilika aliwasilisha kwao, mwaka 2009.

Ameongeza kwamba hadi anaondoka TBC hakuna mtu yoyote aliyezungumzia suala hilo, si Serikali wala bodi.

Tido alipoulizwa na  wakili Swai juu ya tofauti za mkataba aliongia na kampuni ya Chanel 2 group na ule wa Startimes alidai yeye aliandikishiana nao mkataba wa makubaliano ya awali kwa sababu walikuwa wakitaka kuhakikishiwa kama wangeitwa na bodi ya TBC na kwamba aliusaini yeye peke yake.

Ameongeza kuwa katika mkataba halisi walioingia na kampuni ya Startimes aliusaini yeye na mwanasheria wa TBC.

Alibainisha kuwa mkataba wa Startimes ndio mkataba halisi ambao waliandikishiana baada ya bodi kuridhia.

Tido amedai kuwa kutokana na sheria na taratibu za  manunuzi, mkataba halali wa TBC lazima usainiwe na watu wawili ambao ni Mkurugenzi na Mwanasheria na pia lazima uwe na muhuri wa shirika.

Na kwamba katika mkataba wa makubaliano ya awali baina  ya TBC  na kampuni ya Channel 2 group ya Dubai aliusaini yeye kwa kuwa walikuwa wanataka kuthibitishiwa.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo tayari umeshafunga ushahidi wake.

Miongoni mwa  mashahidi  wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi  katika kesi hiyo ni pamoja na  ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.

Katika kesi hiyo inadaiwa Juni 16, 2008, akiwa  Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE),  Tido kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa  Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast  Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho,  anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC  hasara ya Sh887,122,219.19. Tido yupo nje kwa dhamana.

Chanzo: mwananchi.co.tz