Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shuhuda aeleza mahakama alivyovyamiwa na Sabaya

84d1e42c8275ef10dd30979e35e75a73 Shuhuda aeleza mahakama alivyovyamiwa na Sabaya

Fri, 30 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHAHIDI wa sita, Bakari Msangi(38) katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha na uporaji mali na fedha zaidi ya Sh 3,159,000 inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili, ameieleza Mahakama jinsi Sabaya na kundi lake la watu zaidi ya 10 wakiwa na bunduki mbili na bastola walivamia nyumbani kwa mfanyabiashara Mohamed Al Saad Hajirini.

Amesema lengo la uvamizi huo lilikuwa ni kumpekuwa mfanyabiashara huyo kwa madai ya kufanya biashara haramu kwani wametumwa na serikali na shughuli hiyo inatambuliwa na kiongozi mkuu wa nchi.

Msangi alitoa ushahidi huo jana akiongozwa na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikal, Tumaini Kweka, mbele ya Hakimu Mwandamizi, Odira Amworo anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya wazi mkoa wa Arusha iliyokuwa imefurika wakazi wa Arusha wenye hamu ya kujua hatma ya kesi hiyo.

Alidai wakati Sabaya na kundi lake wanavamia nyumba ya Hajirini iliyopo Makao Mapya nyuma ya stendi ya Dar Express katika nyumba za Shirika la Nyumba (NHC), yeye alikuwa amefungwa pingu mkononi baada ya pingu ya mguuni kufunguliwa na walinzi wa Sabaya wakiongozwa na mmoja wa walinzi wake aliyemtambua kwa jina moja la Andrew.

Shahidi alidai walipofika getini katika nyumba hiyo inayolindwa na askari wa kampuni binafsi, alimsikia Sabaya akijitambulisha kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Hai amekwenda katika nyumba hiyo kumsaka Hajirini na kumpekua katika nyumba yake na kwamba yuko hapo kikazi kwa kuwa serikali inajua na zaidi kiongozi wa nchi, Rais Dk John Magufuli ana taarifa zote na baraka hiyo amempa.

Alidai askari hao walimruhusu Sabaya kuingia ndani akiwa na kundi lake wakiwa na silaha hizo na baada ya muda alisikia ukunga wa sauti kubwa wa kike kutoka katika nyumba hiyo wakati yeye akiwa na dereva katika gari huku amefungwa pindu za mikononi.

Alidai Februari 16, mwaka huu aliitwa polisi na Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arusha aliyemtambua kwa jina moja la Gwakisa ili kuwatambua waliompiga na kuvamia duka la Shahidi Store na aliwatambua katika gwaride la utamhulisho katika makundi mawili moja likiwa na watu tisa alimtambua mshitakiwa wa tatu Daniel Mbura (38) na Deogratus Peter , lakini alishanga kutomwona mtuhumiwa mwingine katika kesi hiyo alitwae Peter.

Shahidi huyo alipotakiwa kwenda kumtambua mahakamani hapo Mbura, alienda moja kwa moja na kumshika bega la kushoto na kusema kuwa huyu alikuwepo katika matukio yote ya uhalifu ya Februal 9 mwaka huu katika maeneo ya Dukani, nyumbani kwa Hajirini,Panoni Supermarket na Tulia Lodge na hakuwa na shaka naye kwani waliomfanyia uhalifu wote anawatambua hata wakiwa hamsini kwenye gwaride la utambulisho.

Akihojiwa na Wakili Mosses Mahuna anayemtetea Mshitakiwa wa kwanza Shahidi alikiri kumsikia kuwa kazi ya kupambana na raia wa Tanzania wenye Asili ya Kiaarabu wenye kufanya biashara ya kubadilisha dola bila kibali,utakatishaji fedha haramu na kuuza bidhaa bila kutoa lisiti ameagizwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya Tano Marehemu Dk John Magufuli.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili Mahuna na Shahidi wa sita katika kesi hiyo

Wakili: Ni Kweli Ally Al Saad Hajirini alikupigia simu na kukuambia kuwa dukani kwa Mohamed Al Saad Hajirini yuko Sabaya anapiga watu

Shahidi: Ndio

Wakili: Ni Kweli watu walikuwa wana mshangaa na kuangalia dukani na kukuonya usiende utakufa

Shahidi: Ni Kweli

Wakili: Ni Kweli ulikanywa hadi lugha ya kipare juu ya wewe kutokwenda dukani wala kuingia

Shahidi: Ndio

Wakili: Kabla hujaingia uliona watu wenye Silaha nje ya duka

Shahidi: Ni Kweli niliwaona

Wakili: Duka la nani

Shahidi: Duka la Mohamed Al Saad Hajirini

Wakili: Ulienda dukani kama diwani

Shahidi: Hapana nilienda kama rafiki na kama Ndugu

Wakili: Hilo eneo lina diwani

Shahidi: Ndio

Wakili: Eneo hilo lina uongozi wa Kata

Shahidi: Ndio

Wakili: Hujui wewe ni mvamizi

Shahidi: Sio Mvamizi

Wakili: Ulipoingia dukani ulimkuta Sabaya

Shahidi: Ndio nilimwona na kumsalimia

Wakili: Unajua kipindi hicho alikuwa Nani

Shahidi: Ndio

Wakili: alikuwa Nani

Shahidi: Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro

Wakili: Unajua Mkuu wa Wilaya ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya

Shahidi: Ndio

Wakili: Unajua Mkuu wa Wilaya ni MsaidiI wa Rais Dk John Magufuli

Shahidi: Ndio ni Mteule wake na kwa nini wasiwasiliane naye

Wakili: Wakiwasiliana wewe Utajua

Shahidi: Siwezi kujua

Wakili: Ulipoingia Dukani Sabaya aliagiza walinzi wake upigwe

Shahidi: Ndio

Wakili: Ni Kweli kabla ya kupigwa ulipekuliwa na walinzi wa Sabaya na kuchukuliwa simu mbili na pesa shilingi 390,000

Shahidi: Ni Kweli

Wakili: Ni Kweli baada ya kupigwa na walinzi,Sabaya alikutishia kwa Silaha

Shahidi: Ni Kweli

Wakili: Ni Kweli alikutishia na Silaha baada ya kukuambia kuwa unamfuata fuata kwa sababu yeye anaagizwa na Rais

Shahidi: Ni Kweli

Wakili: Kuna wakati Sabaya aliagiza uibiwe simu na pesa

Shahidi; Hapana

Kesi hiyo inaendelea tena Leo kwani Sabaya na wenzake wawili Silvester Nyengu(26) na Daniel Mbura(38) wanashitakiwa kupora Mali na Fedha zaidi ya shilingi Milioni 3,159,000 kwenye duka la Shahiid Store lililopo mtaa wa Bondeni duka hilo linalomikiwa na Mohamed Al Saad.

Chanzo: www.habarileo.co.tz