Watu watano, akiwemo Mtingwa Kilimanjaro, maarufu kama Shetani, Mkazi wa Mbamba, mwenye umri wa miaka 42, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza, leo Januari 19,2024 na kusomewa shtaka la mauaji ya Sophia Maduka (61) na mumewe Mathias Lusesa (73), wote wakazi wa Lwenge wilayani humo.
Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Tumsifu Barnabas, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Mkaguzi wa Polisi, Martha Chacha amewataja washtakiwa wengine kuwa ni Majaliwa Damasi (18) Mkazi wa Masumbwe, Emmanuel Damasi (34) Mkazi wa Bulungwa, Selina Mchele (49) Mkazi wa Lwenge na Maneno Mashauri (19) Mkazi wa Lwenge.
Martha ameiambia Mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Oktoba 12, 2023 huko Lwenge, Bukokwa wilayani Sengerema, kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Hata hivyo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote na kurejeshwa rumande kutokana na Mahakama hiyo kukosa Mamlaka kisheria ya kusikiliza shauri hilo, huku Hakimu Barnabas akiahirisha kesi hiyo hadi Februari 01, 2024.