Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sheikh ataka wanaume wanaokutwa na hatia ya kubaka, kuwapa mimba wanafunzi wahasiwe

64901 Pic+sheikh

Mon, 1 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Imamu Msaidizi wa Msikiti Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Katanga amesema adhabu ya kifungo cha miaka 30 au maisha jela kwa watuhumiwa wanaokutwa na hatia ya kubaka, kulawiti na kuwapa mimba wanafunzi inaonekana kutokuwa suluhisho la kukomesha vitendo hivyo, kutokana na kuendelea kushamili kwenye jamii.

Amesema wao kama viongozi wa dini wanaona ipo sababu kubwa kumfikishia wazo Rais, John Magufuli la kutungwa sheria ya kuhasiwa kwa wanaume wanaokutwa na hatia ya kulawiti, kuwabaka, kuwapa mimba wanafunzi na kufanya vitendo vya kikatili kwa watoto badala ya kufungwa  miaka 30 au maisha jela.

Sheikh Katanga ameyasema hayo Jijini Mbeya juzi, Juni 28, 2019 wakati akizungumza kwenye kusanyiko la watoto wanaolelewa kwenye vituo vya kulelea yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya  siku ya Mtoto wa Afrika lililokuwa limeandaliwa na Dawati la Jinsia la Polisi Mkoa wa Mbeya na kufanyika viwanja vya FFU jijini Mbeya.

 

Amesema kama viongozi wa dini wana wazo la kumfikishia Rais Magufuli itungwe sheria ya kuwahasi wanaume wanaokutwa na hatia ya kuwafanyia vitendo viovu watoto kwani sheria ya sasa ya kufungwa kifungo cha miaka 30 jela maisha gerezani inaonekana kuzoeleka na kutoogopeka ndio maana vitendo hivyo bado vinaendelea kushamiri kwenye jamii.

“Viongozi wa dini tunajaribu kulifikiria na tuna wazo kwamba  tumfikishie mheshimiwa Rais wetu John Magufuli, kwamba ni vizuri jambo hili lipitishwe, mwenye kufanya tabia chafu na mbaya kwa watoto wetu, badala ya kuwafunga  miaka 30  au maisha jela ni vizuri watu hawa wakahasiwa. Hiyo ndiyo fikra ambayo sisi tunaifikiria,” alisema Sheikh Katanga.

Pia Soma

 

  Amesema adhabu ya sasa ya kumfunga jela miaka 30 au maisha gerezani ni sawa na kumpa mzigo mwananchi wa kumtunza mtu huyo kwani akiwa gerezani atalazimika kutunzwa kwa kodi zinatokana na Watanzania.

Amesema ‘Unamtunza namna gani… kodi tunayotoa ndiyo inamtunza mtu yule kwani anakuwa akiwa gerezani. Sasa katuharibia mtoto, ameharibu mazingira rafiki na malengo yake ya mbele ya huyu mtoto lakini bado tena tunakuwa na suala zima la kumtunza na kumlea mtu huyu kwa miaka yote atakayoishi gerezani akila nguvu za Watanzania kupitia kodi zetu. Hii inaumiza sana’.

Amesema  ni vyema wanaume hao wakikutwa na hatia basi wapewe adhabu ya kuhasiwa halafu waachwe huru kwani ni adhabu tosha na  hatarudia tena mchezo huo na itakuwa ni fundisho kwa watu wote wenye mtazamo wa kuwabaka, kuwalawiti na kuwafanyia vitendo viovu watoto.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema suala la ubakaji, ulawiti na ukatili kwa watoto mkoani hapa unachangiwa zaidi na imani za kishirikina kwa lengo la kutafuta utajiri na mali.

Amsema ‘Suala la unyanyasaji wa watoto ni mkubwa sana katika jamii yetu ya Mkoa wa Mbeya. Lakini niseme jeshi la polisi lipo makini na tunasema watu wa namna hiyo hatutawavumilia hata kidogo.

Imani za kishirikina zinachangia mno ukatili wa watoto, waganga wa jadi wanawaraghai watu kwamba kama unataka utajiri basi nenda kambake mtoto, au kalete kiungo cha mtoto mdogo, sasa hawa watu tumeacha kuchukua hatua kali dhidi yao’.

 

Amesema pamoja na hatua kali zinazochukuliwa kwa watu wanaobainika kufanya vitendo viovu kwa watoto, lakini polisi kupitia dawati lake la jinsi wanaendelea hatua mbalimbali ikiwamo kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki na usalama wa mtoto, na wamefungua madawati maalumu ya kushughulikia watoto wilayani kwa lengo la kuifikia jamii nzima ya Mkoa wa Mbeya.

Mdau wa masuala ya watoto, Muuguzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Shida Kadodo amesema pamoja na jeshi la polisi kuendelea kupambana na ukatili wa kijinsia kwa mtoto, lakini bado jukumu la kuhakikisha usalama na haki za mtoto ni la wazazi au walezi.

Amesema, “Ndugu zangu, usalama na malezi bora ya mtoto upo mikononi mwa sisi wazazi hasa sisi kina mama, tusiruhusu kirahisi rahisi tu watoto wetu eti kulala na wajomba, kaka au hata baba. Tuwe karibu na watoto wetu muda wote licha ya ‘ubusy’ wetu na majukumu ya kazini lakini lazima tujijengee utamaduni wa kukaa watoto wetu hata kwa muda mfupi tu ukitoka kazini kwako na sio kumuachia mfanyakazi wa ndani kuwa ndio  mlinzi na mlezi wa watoto wako.”

Awali, Mkuu wa dawati la jinsia la polisi wilaya ya Mbeya Mjini, Inspekta Veronica Ponera amesema katika kupambana na kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa watoto, wanakumbana na changamoto ya wazazi kujenga usiri na kutokuwa tayari kutoa taarifa wala ushirikiano pindi mtoto anapokuwa amefanyikiwa kitendo cha kikatili.

Amesema, “Unakuta mtoto kalawitiwa au kabakwa na mjomba au na mtu wa karibu na familia fulani, sasa badala ya wazazi wa mtoto huyu kutoa taarifa polisi ili hatua zichukuliwe wao huficha na kutaka kumalizana wao kwa wao.”

 Sasa hili tunaomba sana wazazi na walezi liepukeni kwani kwanza kufanya hivyo kosa kwenu nyote, lakini pia ni kutomtendea haki ya msingi huyu mtoto aliyefanyiwa kitendo hiki kiovu. Lakini pia tunaendelea kukutana na jamii kutoa elimu bila kuchoka na hatua nyingine pia.”

Chanzo: mwananchi.co.tz