Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi wa sita akwamisha kesi ya kina Mbowe

Muuza Mbegepic Shahidi wa sita akwamisha kesi ya kina Mbowe

Wed, 3 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu imeahirishwa baada ya shahidi wa Jamhuri kushindwa kufika mahakamani kwa madai ya tatizo la kiafya.

Shahidi huyo wa sita alitarajiwa kuanza kutoa ushahidi leo Jumatano Novemba 3, 2021 katika Mahakama Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Robert Kidando, aliiomba Mahakama iahirishe kesi mpaka kesho kwa kuwa shahidi wao amepata tatizo la kiafya.

“Shauri linakuja kwa ajili ya kusikilizwa. mpaka jana kuna shahidi ambaye tulikuwa tumepanga kuendelea naye lakini amepata tatizo la kiafya. Hivyo tunaomba ahirisho mpaka kesho tutakapoweza kuendelea. Suala hili liko nje ya uwezo wetu” Kidando.

Upande wa utetezi walikubali ombi hilo “Kwa kufuata amri ya Mahakama ya jana sisi tulikuwa tumejiandaa lakini kwa kuwa mambo yako hivi hatuna namna ila tunaomba tu wenzetu wajitahidi kesho tarehe 4 tuweze kuendelea.” wakili Peter Kibatala.

Jaji Joachim Tiganga ameahirisha kesi hiyo hadi Kesho Alhamisi Novemba 4, 2021.

“Kufuatia maombi ambayo yameletwa na wakili Serikali kwamba shahidi waliyekuwa wamemwandaa amefika mahali hawezi kuja kutoa ushahidi kwa sababu zilizoelezwa za kiafya na kwa kuzingatia kuwa upande wa utetezi haukupinga basi maombi haya yanakubaliwa na shauri hili linaahirishwa hadi kesho.

“Upande wa mashtaka mnakumbushwa kuanda mashahidi ili tuweze kuendelea. Washtakiwa mtaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Magereza” Jaji Tiganga.

Mbowe anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kupanga kutekeleza ugaidi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan (mshtakiwa wa kwanza), Adamu Hassan Kasekwa maarufu Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Katika kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021, Mbowe anadaiwa kufadhili mipango ya kutekeleza ugaidi kwa kutoa fedha kwa washtakiwa wenzake.

Chanzo: mwananchidigital