Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi wa pili kutoa ushahidi leo kesi ndogo ya kina Mbowe

LEO MBOWE Shahidi wa pili kutoa ushahidi leo kesi ndogo ya kina Mbowe

Fri, 12 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Shahidi wa pili upande wa mashtaka katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu anatarajia kuanza kutoa ushahidi leo Ijumaa Novemba 12, 2021.

Ushahidi huo unatolewa katika Mahakama ya Kuu ya Divisheni ya Makosa Rushwa na Uhujumu Uchumi kudhibitisha maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo Mohamed Ling'wenya ambayo upande wa utetezi walipinga yasipokewe na mahakama hiyo.

Jana, mawakili wanaomtetea Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na makosa ya ugaidi walipata ahueni kwa mara ya kwanza pale mahakama ilipokataa kupokea kitabu cha kumbukumbu za mahabusu kama kielelezo cha kesi hiyo.

Jaji Joachim Tiganga alikataa kupokea kilelezo hicho baada ya kuridhika na hoja za utetezi kuwa shahidi aliyetaka kukitoa alishindwa kueleza ni kwa namna gani kilimfikia.

Uamuzi huo umekuja kufuatia pingamizi la utetezi lililowekwa juzi wakati wa usikilizwaji wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.

Kesi hiyo inamkabili Mbowe na watu wengine watatu waliowahi kuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kikosi cha makomandoo, Ngerengere, kabla ya kuachishwa kazi kwa sababu za kiafya.

Kesi hiyo ndogo iliibuka baada ya mawakili wa utetezi kupinga kupokewa kwa maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohamed Ling’wenya kwa madai kuwa hakuwahi kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam anakodaiwa kuchukuliwa maelezo.

Mawakili hao walidai pia mshtakiwa huyo alilazimishwa kusaini maelezo yaliyokuwa yameandaliwa huku akitishwa.

Chanzo: mwananchidigital