Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi wa nane kesi ya kina Mbowe leo

Mbowepic Shahidi 8 Shahidi wa nane kesi ya kina Mbowe leo

Mon, 8 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Baada ya mapumziko ya mwisho wa wiki, leo kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu inaendelea.

Mbowe na wenzake wanashtakiwa kwa tuhuma za ugaidi, kesi inayoendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam.

Katika mwendelezo huo, upande wa mashtaka unatarajiwa kuendelea kutoa ushahidi na Mahakama inatarajiwa kupokea ushahidi wa shahidi wa nane kati ya mashahidi 24 .

Shahidi wa mwisho kabla ya leo (wa saba) alikuwa Inspekta Mahita Omar Mahita, aliyetoa ushahidi wake Ijumaa iliyopita. Inspekta Mahita alikuwa miongoni mwa kikosi cha maofisa wa Polisi kutoka Arusha kilichowatia mbaroni washtakiwa wawili katika kesi hiyo.

Kulingana na aina ya ushahidi wake, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala alitumia saa 2:25 kumhoji maswali mbalimbali shahidi huyo kuhusiana na ushahidi wake, muda ambao ni mrefu zaidi kutumiwa na wakili mmoja kumhoji shahidi tangu kesi hiyo ianze kusikilizwa Septemba 15, mwaka huu.

Wakili Kibatala alilieleza Mwananchi kuwa alitumia muda mwingi zaidi kumhoji shahidi huyo kuliko mashahidi wengine kutokana na ushahidi wake ambao alisema uligusa maeneo mengi.

Alieleza mashahidi wengine ambao itakapofika zamu yao kutoa ushahidi atatumia muda mwingi kuwabana kwa maswali ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jumanne na Koplo Goodluck, ambao pia walikuwa katika timu hiyo iliyowatia mbaroni watuhumiwa, pamoja na Luteni Denis Leo Urio.

Luteni Urio ni Ofisa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), kutoka kikosi Maalum (Special Force) au 92 KJ yaani kikosi cha makomandoo, kilichoko Ngerengere eneo la Sangasanga mkoani Morogoro.

Huyu ni shahidi katika kesi hiyo, kwani mujibu wa maelezo ya maandishi ya mashahidi wa upande wa mashtaka, ndiye anadaiwa kuhusika kuibua tuhuma zinazowakabili washtakiwa.

Wakati kesi hiyo ikisubiriwa kuendelea leo, swali na ama shauku ya wadaawa, hususan washtakiwa na mawakili wao pamoja na wadau wanaofuatilia kesi hiyo ni kujua ni nani shahidi wa nane na kusikia ni ushahidi gani atakaoutoa.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Washtakiwa hao watatu walikuwa askari wa JWTZ, 92 KJ, Ngerengere ambao waliachishwa kwa sababu za kinidhamu.

Chanzo: mwananchidigital