Shahidi wa 12, Sabri Sharif (36) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa alipokwenda kumuuzia gari aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya alimkuta akiwa na watu zaidi ya sita.
Shahidi huyo wa Jamhuri aliyasema hayo jana, wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake mahakamani hapo.
Aliieleza Mahakama kuwa yeye ndiye aliyemuuzia Sabaya gari aina ya Toyota Land Cruiser, kwa thamani ya Sh60 milioni.
Pia, alimtaka Sabaya amlipe fedha zake zilizosalia Sh200,000 zilizobaki kwenye gharama za kubadili jina la umiliki wa gari.
Mbele ya Hakimu Mkazi Patricia Kisinda, Jamhuri iliwakilishwa na jopo la mawakili sita, wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka huku upande wa utetezi ukiwa na mawakili wanne.
Akiongozwa na Kweka, shahidi huyo ambaye ni mfanyabiashara wa magari katika kampuni ya Sharija Motors, Kinondoni jijini Dar es Salaam, aliieleza Mahakama kuwa alikutana na Sabaya Februari 2, 2021 katika “appartment za Blackwood” zilizopo jijini humo.
Advertisement “Nilimkuta Sabaya akikagua nyaraka, ikiwamo kadi ya gari na mkataba nilionunulia gari kutoka Kampuni ya Oil Com. Na alikuwapo pia Sylvester Nyegu (mshtakiwa wa tano) aliyejitambulisha kama msaidizi wa Sabaya.”
Alidai kuwa wengine waliokuwapo ni mshtakiwa wa tatu, Watson Mwahomange, ambaye alimsindikiza baada ya kulipwa fedha taslimu na Sabaya.
“Wakati mchakato wa malipo unaendelea, Sabaya alimleta mwanasheria wake tukaanza kuandaa mkataba na akaniacha akaondoka na Sylvester na dereva aitwaye Antorio, wakasema wanakwenda Mlimani City kuweka hela.”
Aliieleza Mahakama kuwa kabla ya siku hiyo, Februari mosi alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Richard, aliyekuwa akimuuliza kuhusu gari hilo ambapo alidai kumueleza ameliuza ila kuna fedha hajamaliziwa.
Shahidi huyo alidai awali alinunua gari hilo kutoka kampuni ya Oil Com na kuliuza Januari 23, mwaka jana kwa Philip Njombe kwa Sh90 milioni, ambapo alikuwa amemlipa Sh70 milioni ikabaki Sh20 milioni.
“Baada ya kupita muda hakufanikisha kulipa kiasi kilichobaki akaanza kutangaza gari analiuza kwa madalali na mitandao ya kijamii, na Sabaya aliliona kupitia dalali wake anayeitwa Richard aliyenipigia simu Februari mosi na kuniuliza kuhusu gari hilo.”
Aliieleza Mahakama kuwa dalali huyo alimwambia aongee na Sabaya, ambaye alimtaka siku inayofuata aende na nyaraka zinazoonyesha anadai pesa hizo na za gari hilo.
Alieleza kuwa baada ya saa mbili, walirejea. Awali Antorio alimtumia karatasi ya kuweka fedha benki (bank slip) ikionyesha walimuwekea Sh39 milioni.
“Sabaya alikuja na Sh21 milioni na kati ya hizo akampa dalali Sh1 milioni na Sh20 milioni akanipa mimi, tukakubaliana atalipa uhamisho wa jina la umiliki wa gari kwa gharama ya Sh700,000.
“Kutokana na mazingira yaliyokuwepo pale na watu kuwa wengi nilimuomba Sabaya nitoke pale nikisindikizwa na mtu, ambapo alinipa yule pale (mshtakiwa wa tatu) akanisindikiza hadi Kinondoni,” alidai shahidi huyo.
Alidai mahakamani hapo kuwa Sabaya alitoa Sh500,000 na kumweleza kuwa atakapokamilisha mchakato wa uhamisho wa jina atampa Sh 200,000 iliyobaki kisha ampe kadi yake, na kudai Aprili 16, 2021 mchakato ulikamilika lakini Sabaya hakummalizia kiasi hicho cha fedha hata alipokutana naye Dodoma.
“Nililazimika kutoa Sh 200,000 zangu na kuchukua ile kadi, nikaja kukutana na Sabaya na Sylvester kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma, nikamfahamisha tena kadi ipo tayari wakaniambia wakimaliza kazi yao watakuja,” alisema na kuongeza:
“Hatujawahi kuonana tena mpaka leo na nitashukuru kama akinilipa deni langu, lakini kadi ya gari niliiacha Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa).”
Sharif aliieleza Mahakama kuwa Juni mosi, mwaka huu aliitwa Makao Makuu ya Takukuru kuhojiwa kuhusu biashara ya gari aliyofanya na Sabaya.