Shahidi wa wa 10 katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake sita leo Novemba 22, 2021 anatarajiwa kutoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha.
Hadi sasa mashahidi tisa wametoa ushahidi mbele ya Hakimu Patricia Kisinda. Upande wa Jamhuri unatarajiwa kuwa na mashahidi 20 katika kesi hiyo.
Mbali na Sabaya washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Silvester Nyengu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31). Katika kesi hiyo Sabaya na wenzake wanakabiliwa na mashitaka matano.
Shitaka la kwanza linaliwakabili washitakiwa wote ilidaiwa kuwa Januari 20 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha na Mkoa wa Arusha Sabaya inadaiwa kuwa akiwa na genge la uhalifu alilokuwa akiliongoza alitumia vibaya akiwa Mkuu wa Wilaya.
Shitaka la pili linamkabili Sabaya akidaiwa kuwa Januari 20 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha na Mkoa wa Arusha alishiriki kuomba rushwa ya shilingi milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara, Francis Mrosso.
Katika shitaka la tatu Sabaya anadaiwa kuomba rushwa ya shilingi milioni 90 kwa Mrosso ili aweze kumsaidia katika kesi ya jinai ya ukwepaji kodi iliyokuwa ikimkabili.
Shitaka la nne linamkabili Sabaya akidaiwa kuwa Januari 20 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha na Mkoa wa Arusha aliomba rushwa ya shilingi milioni 90 kutoka kwa Mrosso.
Katika shitaka la tano la utakatishaji fedha haramu linawakabili washitakiwa wote wakidaiwa kuwa Januari 20 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha na mkoa huo walichukua fedha shilingi milioni 90 kwa Mrosso na kwenda kuzifanyia matumizi yasiyokuwa halali kinyume na sheria ya utakatishaji fedha.