Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi kesi ya vigogo TRA aeleza alivyotoa nakala za michoro ya mabehewa

70432 TRL+pic

Thu, 8 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Albert Maganyi, shahidi  katika  kesi ya matumizi mabaya ya madaraka  inayowakabili vigogo 11 wa Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) ameileza mahakama jinsi  alivyoipatia  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nakala kivuli ya michoro ya mabehewa ya kokoto badala ya nakala halisi.

Maganyi ambaye ni kaimu mhandisi mitambo  wa Shirika la Reli Tanzania(TRC) ameeleza hayo leo Jumatano Agosti 7, 2019 wakati akitoa ushahidi wake katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi huku akiongozwa na wakili wa Takukuru, Maghela Ndimbo

Vigogo hao  11 wa TRL wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kukiuka sheria wakati wa ununuzi wa mabehewa 25.

Amedai Desemba Mosi, 2015 akiwa ofisini kwake alipewa maelekezo kutoka kwa aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu kuwa awape Takukuru  michoro halisi ya mabehewa ya kokoto.

Maganyi amedai kuwa michoro aliyowakabidhi Takukuru ilikuwa  ni nakala na alipojaribu kufuatilia michoro halisi ya mabehewa ya kokoto alielezwa kuwa ilichukuliwa na kamati ya awali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

“Nilimfuata Dk Kailembo na aliyekuwa mkuu wa ufundi na meneja ujenzi, Ngoso Ngosomwile walimweleza kuwa michoro halisi ya mabehewa ya kokoto imechukuliwa na kamati ya awali kwa ajili ya kuichunguza,” amedai Maganyi.

Pia Soma

Amedai kuwa michoro hiyo ilisainiwa na aliyekuwa kaimu mhandisi wa ufundi na meneja ujenzi, Muungano Kaupunda na mhandisi mkuu wa ufundi, Paschal Mafikiri.

Maganyi amedai kuwa michoro hiyo aliwakabidhi Takukuru kwa kutumia hati ya makabidhiano hivyo aliiomba mahakama hiyo ipokee vielelezo vitumike  kwenye ushahidi wake.

Baada ya maelezo hayo upande wa utetezi walipinga visipokelewe kwa kuwa hakufuata sheria.

Hakimu Shaidi ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 16, 2019 ka ajili ya kujibu pingamizi hilo.

Vigogo katika kesi hiyo ni aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu;  mkuu wa kitengo cha makenika na mhasibu mkuu,  Jasper Kisiraga; kaimu meneja wa usafiri, Mathias Massae; kaimu mhandisi wa ufundi na meneja ujenzi, Muungano Kaupunda na mkuu wa ufundi na meneja ujenzi, Ngoso Ngosomwiles.

Wengine ni mhandisi mkuu wa ufundi, Paschal Mafikiri; mhandisi mipango,  Kedmo Mapunda; kaimu mhandisi wa mawasiliano, Felix Kashaingili;  mkuu wa usafiri wa reli, Lowland Simtengu; mkuu wa ubunifu na utengenezaji wa nyaraka, Joseph Syaizyagi na kaimu mkuu wa usafirishaji, Charles Ndenge.

Chanzo: mwananchi.co.tz