Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi kesi ya mke wa bilionea Msuya aeleza eneo mauaji yalikopangwa

Mke Wa Msuya Shahidi kesi ya mke wa bilionea Msuya aeleza eneo mauaji yalikopangwa

Fri, 4 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi katika kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella jana ameieleza mahakama jinsi mtuhumiwa alivyowapeleka Kigamboni jijini Dar es Salaam na kuwaonyesha maeneo waliyokuwa wakikutana kupanga mauaji hayo.

Mrita na Muyella wanadaiwa kumuua kwa kumchinja dada wa marehemu Msuya, Aneth Msuya nyumbani kwake Kibada, Kigamboni Mei 25, 2016 huku mwanawe wa miaka minne, Allan Kimario akidaiwa kushuhudia.

Jana, shahidi wa tano wa Jamhuri, SP Latifa Mohamed (42) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Kanda Maalumu ya Kipolisi, Dar es Salaam, ameieleza Mahakama Kuu kuwa Mrita aliwaeleza anakumbuka eneo la Kigamboni walipokuwa wakikutana wakati akimhoji na angeweza kuwapeleka.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Genes Tesha, mbele ya Jaji Edwin Kakolaki, shahidi huyo alidai Agosti 8, 2016 alipewa jukumu la kumhoji Miriam kwa njia ya mdomo na wakati huo mahojiano hayo yakirekodiwa kwa video.

“Nilijitambulisha na kumueleza tunachotaka kufanya na yeye alikubali kurekodiwa na baada ya mahojiano tulimuuliza kama Kigamboni anapafahamu na akajibu anapakumbuka.

“Tulimuuliza kama anaweza kutupeleka akasema ndiyo, kisha tuliondoka na kuelekea Kigamboni, alituelekeza tukashuka na kurekodi eneo waliokuwa wanakutana,” alisema.

Alidai baada ya shughuli hiyo walirudi Kituo cha Polisi Chang’ombe na mtuhumiwa alirudishwa mahabusu.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili wa utetezi, Peter Kibatala na shahidi huyo wa Jamhuri, Latifa Mohammed.

Kibatala: Wewe ulikuwa mpelelezi kwenye hii kesi?

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Majukumu yako yalikuwa ni nini?

Shahidi: Ukamataji.

Kibatala: Unafahamu ukamataji unaongozwa na sheria?

Shahidi: Ndiyo.

Kibatala: Wakati unaenda Arusha ulijua unaenda kukamata?

Shahidi: Ndiyo.

Kibatala: Kwa hiyo haikuwa dharura?

Shahidi: Ndiyo.

Kibatala: Mlikuwa na David Mhang’aya?

Shahidi: Ndiyo.

Kibatala: Mlikuwa pia na Jumanne Malaghahe?

Shahidi: Ndiyo.

Kibatala: Ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arumeru?

Shahidi: Ndiyo.

Kibatala: Unafahamu anajulikana nchi nzima kwa tuhuma za utesaji?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Kwenye kesi namba 63/2021 mtuhumiwa wa kwanza na wa pili walimtaja kuwa aliwatesa walipokamatwa?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unamfahamu Mahita Omar Mahita?

Shahidi: Namfahamu.

Kibatala: Yuko wapi kwa sasa.

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Wakati wa utekelezaji wa majukumu yenu mlikuwa mnapokea amri kutoka kwa nani?

Shahidi: Afande David.

Kibatala: Hujawahi kupewa maelekezo na wewe ukarudisha kwa RCO Richard Mchomvu?

Shahidi: Sijawahi.

Kibatala: Kwa uelewa wako baada ya kufika Dar taarifa zilipelekwa kwa RCO au DCI?

Shahidi: Kwa RCO.

Kibatala: Unafahamu ukamataji unaongozwa na sheria?

Shahidi: Ndiyo.

Kibatala: Unafahamu hati ya ukamataji?

Shahidi: Ndiyo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 8 mwaka huu ambapo shahidi mwingine wa Jamhuri atatoa ushahidi.

Tayari mashahidi watano kati ya 45 wanaotarajiwa kuitwa na wa upande wa mashtaka wamekwishatoa ushahidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live