Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi kesi ya mihadarati ya Kiboko aeleza alivyoshughulikia vielelezo

Cc0ed0dcf86fde42a423cdf211ed29dd.jpeg Shahidi kesi ya mihadarati ya Kiboko aeleza alivyoshughulikia vielelezo

Sat, 28 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHAHIDI wa tatu katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya inayomkabili mfanyabiashara Ayubu Kiboko na mkewe Pili Kiboko ameendelea kutoa ushahidi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Kanda ya Dar es Salaam na kueleza namna upekuzi ulivyofanyika, kukamata vielelezo ikiwemo vikopo vyenye unga uliodhaniwa kuwa dawa za kulevya.

Shahidi huyo, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Emmanuel Ambikile alitoa ushahidi wake mahakamani hapo mbele ya Jaji Lilian Mashaka akiongozwa na Wakili wa Serikali, Kanditi Nasua na Wakili wa utetezi, Majura Magafu.

Katika ushahidi huo, Ambikile alidai Mei 23, 2018 alipokea hati ya ukamataji wa vielelezo uliofanyika nyumbani kwa mshtakiwa maeneo ya Tegeta Nyuki jijini Dar es Salaam.

Alidai katika upekuzi huo ambao ulishuhudiwa na watu aliowataja kwa majina ya Christina Macha na Raimond Kimambo, askari walikamata bastola moja aina ya Brown na risasi saba.

Pia kasha la kutunzia bastola, simu aina ya Nokia, Kadi ya benki ya CRDB, kadi ya benki ya Umoja, fomu ya kuweka fedha, faili ndogo yenye nyaraka, faili za TRA(Mamlaka ya Mapato Tanzania), redio call na hati za kusafiria tatu za mshtakiwa.

Alidai pia walikuta kikopo angavu cha plastiki chenye unga mweupe, nailoni nyepesi yenye chenga chenga za unga, hati nne za kusafiria zenye majina yake, ya mke wake na watoto wao, kadi mbili za gari aina ya Prado, kadi moja ya gari aina ya Toyota Hilux na kitabu cha silaha.

Alidai baada ya kupokea hati na vielelezo, Ambikile aliweka alama katika vielelezo hasa vile vilivyodhaniwa kuwa dawa za kulevya kwa ajili ya kuchukua hatua nyingine ambapo waliondoka navyo kwenda Ofisi za Mamlaka ya Dawa za Kulevya (DCEA).

Walifika DCEA saa 2:00 asubuhi na kukabidhi vielelezo kwa ofisa anayetunza vielelezo, SSP Neema ambavyo walitilia shaka kuwa ni dawa za kulevya huku yeye akibaki na vile ambavyo havihusiani na dawa za kulevya.

Akiongozwa na wakili wa utetezi Majura Magafu, Ambikile alidai walipofika nyumbani kwa mshitakiwa walimkuta akiwa na mkewe na mabinti wengine ambao alidai hawakuwahoji kwa sababu mshtakiwa alidai hawahusiki.

Aidha alipoulizwa kama vielelezo vilivyodhaniwa kuwa dawa za kulevya vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu, Ambikile alidai hajui chochote kuhusu hilo.

Chanzo: habarileo.co.tz