Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi kesi ya Zumaridi adai alipokamatwa aliunganishwa na watu asiowajua

Zumaridiipic Data Shahidi kesi ya Zumaridi adai alipokamatwa aliunganishwa na watu asiowajua

Thu, 24 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa kwanza wa utetezi katika kesi ya Jinai namba 10/2022 inayomkabili Diana Bundala maarufu 'Mfalme Zumaridi' na wenzake nane, Amos Kailembo ameieleza mahakama alikamatwa na kuunganishwa na watu asiowajua katika kesi hiyo.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza, Mfalme Zumaridi na wenzake wanakabiliwa na shataka la kufanya kusanyiko lisilo halali.

Akiongozwa na Wakili wa utetezi, Erick Mutta, Kailembo ambaye pia ni mshtakiwa namba 2 katika kesi hiyo ameileza mahakama hiyo leo Jumatano, Novemba 23,2022 kuwa Februari 26 mwaka huu alikuwa akifanya kibarua cha ujenzi nyumbani kwa Mfalme Zumaridi katika Mtaa wa Buguku kata ya Buhongwa jijini Mwanza ghafla polisi waliingia na kumkamata.

Aidha, Kailembo ameeleza baada ya kukamatwa na Askari Polisi aliunganishwa na watu wengine ambao hakufahamu makosa yanayowakabili huku akikana maelezo ya onyo yaliyowasilisha na upande wa mashtaka mahakamani hapo kuwa siyo ya kwake.

"Hata maelezo ya onyo ambayo yaliwasilishwa na mwendesha mashtaka wa Serikali mahakamani hapa siyo ya kwangu ndiyo maana niliyakataa tangu mwanzoni," ameeleza Kailembo

Isaya Yusuph ambaye ni shahidi wa pili na mshtakiwa namba 3 kwenye kesi hiyo, ameieleza mahakama naye pamoja na kuwa katika nyumba ya mhubiri huyo akimsaidia fundi aliyekuwa anajenga alikamatwa kisha kuunganishwa na washtakiwa wengine.

Pia, amekana kuwahi kumuona Mfalme Zumaridi kabla ya kukamatwa Februari 26, 2022 huku akidai baada ya kukamatwa ndipo alimuona mhubiri huyo walipofikishwa kituoni.

Katika hatua nyingine, kesi ya Jinai namba 11/2022 inayomkabili Diana Bundala peke yake imetajwa mahakamani hapo huku mwendesha mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Martha Mwadenya akiieleza mahakama upelelezi wake haujakamilika.

Majibu ya kutokamilika kwa upelelezi huo yakamuibua wakili wa utetezi, Erick Mutta aliyedai mteja wake amechoshwa na kauli ya upelelezi kutokamilika huku akiiomba mahakama ihoji kwa nini upelelezi haukamiliki.

"Mteja wangu anasema ni miezi sita tangu akamatwe bila hata kupatiwa dhamana matokeo yake kumekuwa na kisingizio cha upelelezi kutokamilika tunaiomba mahakama yako tukufu ihoji upande wa mashtaka ni lini utakamilika," ameeleza Mutta

Baada ya mvutano huo, Hakimu Mkazi Mkuu, Monica Ndyekobora akahairisha kesi hiyo hadi kesho Jumatano Novemba 24, 2022 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa utetezi huku akimtaka wakili, Mutta afuatilie maombi yao katika Mahakama Kuu kwani mahakama hiyo haina nguvu ya kisheria ya kusikiliza kesi inayomkabili mhubiri huyo.

Katika kesi hiyo, Mfalme Zumaridi anakabiliwa na shtaka la usafirishaji haramu wa binadamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live