Dar es Salaam. Shahidi wa tano katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliwatibu majeruhi watatu wanaodaiwa kuwaua askari polisi wawili.
Shahidi huyo, Ernest Nsumila (46), ambaye ni daktari wa kituo cha afya Nguruka cha Wilaya Uvinza mkoani Kigoma, ameieleza mahakama hiyo leo Jumanne Julai 16, 2019 wakati akitoa ushahidi wake.
Akiongozwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Nassoro Katuga, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi, Dk Nsumila amedai Oktoba 18, 2018 akiwa kituo cha afya cha Nguruka alipokea majeruhi watatu ambao wote ni wanaume.
" Nilikuwepo kazini tangu asubuhi ilipofika saa 12 jioni nilipokea majeruhi watatu, wote wanaume wanaotokea kijiji cha Mpeta wakidai wamepigwa risasi na askari polisi kwa madai kuwa walikuwa wanawahamisha maeneo ambayo hayatakiwi kufanya kilimo.”
“Niliwahoji wameenda polisi kuchukua PF3 wakasema hapana. Ikabidi mimi niwaambie ndugu zao waliowaleta waende polisi ili wakachukue hizo PF3, wakati huo nilianza kuwapatia huduma ya kwanza kwa kuwatundikia dripu ya maji na kuwapatia dawa za maumivu kutokana na hali zao kuwa mbaya,” amesema shahidi huyo ambaye aliajiriwa kuwa daktari tangu mwaka 2002.
Amedai majeruhi hao walikuwa na majeraha ya risasi huku wakiwa hawawezi kusimama vizuri na kuongea na kwamba katika kuwahoji zaidi, walisema wamepigwa risasi na polisi katika pori la Mwanduhubandu lililopo kijiji cha Mpeta, wilaya ya Uvinza
Pia Soma
- ATCL kuzindua safari ya Mumbai leo
- Bongo movie, Swahilflix kumleta Will Smith Tanzania
- Rais Magufuli asisitiza bei elekezi zao la pamba ni Sh1,200
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Kono Mwandu, Shishi George na Jumanne Jackson ambao walipelekwa kituoni hapo na ndugu zao.
Dk Nsumila amedia kuwa majeruhi hao wanadaiwa kupigwa risasi na askari polisi katika mapambano baina ya wananchi na polisi, wakati wakihamishwa kutoka katika pori hilo ambalo wananchi hao walikuwa wanafanya shughuli za kilimo.
Shahidi huyo amedai alianza kufanya kazi kituoni hapo tangu 2017 na katika kituo hicho wapo madaktari watatu na wauguzi wachache.
Amedia baada ya muda mfupi, askari polisi walipata taarifa za wajeruhi hao kwenda katika kituo hicho cha afya cha Nguruka, bila kuwa na PF3 na hivyo kuwafuatilia.
Dk Nsumila ambaye siku hiyo alikuwa yeye peke yake pamoja na wauguzi amedai baada ya majeruhi hao kupata nafuu polisi walikuja kuwachukua wodini na kuondoka nao kwa madai kuwa ni wahalifu na kwamba wanaendelea na taratibu za kipolisi.
Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 13 na 14, 2019 itakapoendelea na ushahidi.
Katika kesi hiyo, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi ambayo anadaiwa kuyatenda Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo.