Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi kesi ya Zitto aeleza alivyosaidia kutafuta miili, silaha zilizopotea

101158 Zitto1+pic Shahidi kesi ya Zitto aeleza alivyosaidia kutafuta miili, silaha zilizopotea

Mon, 6 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shahidi wa sita wa upande wa utetezi katika kesi  inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alivyoshirikiana na kamati ya ulinzi na usalama kutafuta miili pamoja na silaha zilizokuwa zimepotea.

Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327 ya mwaka 2018.

Shahidi huyo, Gerald Ibrahim (32)  ambaye ni mfanyabiashara na mkulima mkazi wa kijiji cha Mpeta Wilaya ya Uvinza ameeleza hayo leo Alhamisi Aprili 2, 2020 wakati akitoa ushahidi.

Akiongozwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Huruma Shahid amedai kuwa baada ya kufanya utafiti alibaini chanzo cha mgogoro huo kilitokana na mkuu wa Wilaya aliyekuwepo kutoa tamko lisilokuwa na tija.

Amedai  usiku wa Oktoba 16 kuamkia 17, 2018 ilisikika milio ya risasi bila utaratibu na hakuna tangazo lolote lililokuwa limetolewa na uongozi wa serikali ya kijiji .

"Baada ya risasi kupigwa wananchi walitawanyika maeneo mbalimbali ikiwemo Uvinza, Ilunde, Mpeta na Mliabibi na wakati huo mimi nilikuwa kijiji cha mpeta,” amedai Gerald.

Pia Soma

Advertisement
Amebainisha kuwa kutokana na risasi kupigwa hovyo kulitokea maafa ikiwemo mtu mmoja kupigwa risasi ya mgongoni na mwingine kupigwa risasi kwenye paja.

"Watu nilioshuhudia wakizikwa ni wanne na Oktoba 19 kuna watoto wawili walifariki baada ya nyumba waliokuwa wakiishi kuchomwa moto na kuungulia ndani,” amedai.

Shahidi huyo aliendelea kudai wakati ametumwa na mkuu wa Mkoa kutafuta bunduki zilizokuwa zimepotea, alishuhudia maiti kati ya 18 na 20 zilizokuwa zimeanza kuharibika.

"Silaha hizi zilikuwa ni za Inspekta Ramadhani na Koplo Mudi ambao walifariki, kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa ilifika kijiji cha Mpeta Oktoba 18 kwa ajili ya kufuatilia miili ya askari hawa wawili, bunduki pamoja na kuleta amani,” amedai.

Amedai kuwa katibu tarafa wa Nguruka alimfuata  na kumueleza kuwa kwa namna wananchi wanavyomuheshimu anaweza kuwasaidia lakini alikataa,  baada ya kupewa somo la uzalendo alikubali na kwenda kukutanishwa na kaimu mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Samson Nyaikanga.

"Waliniweka pembeni na kunisihi kushirikiana nao nikajitoa kwa kutoa ushirikiano ili kufika eneo la tukio na kutoa miili ambayo ilikuwa imepatikana,” amesema.

Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi anayodaiwa kutenda Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za  makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo

Chanzo: mwananchi.co.tz