Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi kesi ya Sabaya asema majalada bado yanachunguzwa

044bbccee0cc1f8fb172bdf4e42af292.jpeg Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai

Thu, 9 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa 11 katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake sita, Shabani Hemed (41), amedai kuna majalada ya uchunguzi yanaendelea kuchunguzwa juu ya tuhuma za Sabaya, huku watuhumiwa wengine wakitafutwa.

Hemedi alidai uchunguzi wa majalada mengine ya kesi yamekamilika na yako kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) yakisubiri kibali ili watuhumiwa wapandishwe mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Shahidi huyo ambaye ni Ofisa Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Makao Makuu, amedai hayo wakati akiulizwa maswali na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Felix Kwetukia baada ya kumaliza kuulizwa maswali ya dodoso ya mawakili wa utetezi wakiongozwa na Mosses Mahuna.

Hemed alidai majalada yanayoendelea kuchunguzwa ni ya Sabaya na watuhumiwa ambao baadhi wapo mahakamani na wengine watatafutwa kwa kuhusika na tuhuma katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

“Baadhi ya majalada uchunguzi kwa upande wa Takukuru umekamilika na yapo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wakisubiri kibali ili watuhumiwa waweze kupandishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili,” alidai Hemed.

Mbele ya Hakimu Patricia Kisinda, alidai alikabidhiwa jalada la kesi ya rushwa ya Sh milioni 90 kwa kumtafuta na kumkamata Sabaya na wenzake baada ya kushindikana kujisalimisha. Alisema walikamatwa Dar es Salaam usiku wa manane.

Alidai Sabaya alipokamatwa hakuwa na fedha taslimu, na walikamatwa Mei 27, mwaka huu na kupandishwa kizimbani Juni 4, mwaka huu. Alikana kuwa walikaa kwa muda wa wiki tatu kabla ya kupandishwa mahakamani kama alivyosema wakati anahojiwa na mawakili wa utetezi.

Aidha, alieleza mahakama kuwa Sabaya na wenzake tangu walipokamatwa na kufikishwa kwa wakuu wake wa kazi, hawakuwahi kupigwa wala kuteswa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Jumanne ijayo ambako shahidi wa 12 anatarajiwa kupanda kizimbani kutoa ushahidi katika kesi hiyo ambayo pia inawahusu washitakiwa Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Silvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live