Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi asimulia polisi alivyopigwa kwa Zumaridi

2d1d3e099d8b30c7f1f283a97f403dd5 Kesi ya Zumaridi imeendelea jijini Mwanza

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa kwanza katika kesi inayomkabili Mhubiri, Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na wenzake, ameieleza mahakama namna washitakiwa hao walivyomshambulia askari polisi na kumzuia asitekeleze wajibu wake.

Shahidi huyo katika kesi hiyo namba 11/2022 ambaye ni Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Nyamagana, Christina Mwisongo (46) aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza jana kuwa, alishuhudia tukio hilo nyumbani kwa Zumaridi.

Mbele ya Hakimu, Monica Ndyekobora, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga alieleza kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kumshambulia ofisa wa polisi, kumzuia asitekeleze jukumu lake na usafirishaji haramu wa binadamu.

Mwisongo alidai washitakiwa walimshambulia Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Nyamagana, James Mgaya aliyekuwa amefuatana naye kutekeleza amri ya Mahakama ya Mwanzo ya Mkuyuni jijini Mwanza.

Alidai mahakama ilimtaka aende nyumbani kwa Zumaridi kumchukua mtoto aliyekuwa anaishi na mama yake, Suzana Ndalawa ndani ya nyumba hiyo.

“Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo lilizuka kundi la watu waliovaa nguo nyeupe na walikuwa wakiunguruma kama simba huku wakitoa macho na kugalagala chini,” alidai.

Alidai watu hao walikuwa wameshikana mikono na waliwazuia maofisa hao kuingia ndani ya nyumba hiyo huku wakiwasogelea hivyo walirudi nyuma.

"Walimkamata Afande James na kumuangusha chini wakaanza kumshambulia wakiwa wanamvuta, kumkanyaga, wakimpiga mateke na kumkwaruza kwa makucha huku wakiwa wamemzingira," alidai.

Shahidi huyo alidai walipatwa na taharuki na kushindwa kumuokoa mwenzao, lakini baadaye alijiokoa na wakaenda getini na kutoka wakarudi kituo cha polisi na kuandika maelezo Februari 25, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwisongo, walikwenda nyumbani kwa Zumaridi kumchukua mtoto aliyehitajika katika Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni kwenye shauri la ndoa lililokuwa likiendelea mahakamani hapo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 19, mwaka huu kwa ajili ya kumsikiliza shahidi wa pili. Awali, upande wa Jamhuri uliieleza mahakama kuwa utakuwa na mashahidi 20 na vielelezo vinne.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live