Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi akwamisha tena kesi ya Zitto

44031 Zittopic Shahidi akwamisha tena kesi ya Zitto

Wed, 27 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe imeshindwa kuendelea kutokana na shahidi kupata dharura.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Saimon amedai leo Februari 27,2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi kuwa kesi hiyo ilipangwa kuendelea kwa hatua ya usikilizwaji lakini shahidi amepata dharura yuko nje ya Dar es Saalam.

“Tulipanga kesi hii iendelee kwa hatua ya ushahidi, lakini shahidi tuliyemwandaa amepata dharura yuko nje ya Dar es Salaam tunaomba tarehe nyingine,” amedai Wakili Wankyo.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala ameiambia Mahakama kuwa kesi hiyo inaahirishwa kwa mara ya pili kutokana na shahidi kutofika mahakamani lakini upande wa mashtaka hawajataja jina la shahidi huyo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu  ameutaka upande wa mashtaka kuleta shahidi Machi 11 kesi hiyo itakapokuja tena.

Katika kesi ya msingi, Zito anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za  makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa siku hiyo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa Wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la polisi alitoa Maneno ya uchochezi.

Alitoa maneno ya uchochezi kuwa "watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata Matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata Matibabu wakawafuata kule wakawaua"

Katika shtaka la pili, Zitto anadaiwa  kuwa oktoba 28,  2018 huko Kijitonyama wilaya ya Kinondoni  katika mkutano huo na wanahabari, mshtakiwa alitoa Maneno ya uchochezi yafuatayo "lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili , taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta Nguruka, Uvinza ni mbaya ni taarifa ambazo zinaonesha wananchi wengi sana wameuwawa, na jeshi la polisi, pamoja na kwamba Afande Sirro wamekwenda kule, halijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi....kama hawa wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi, kuna taratibu za kisheria za kuchukua nasiyo kuwauwa,wananchi  wengine sana wamekufa"

Katika shtaka la tatu, mshtakiwa huyo siku hiyo katika mkutano huo huo alitoa waraka kwa umma ukiwa na Maneno ya kichochezi kwa nia ya kuleta chuki kwa watanzania dhidi ya polisi.

Kabwe alitoa waraka huo wenye maneno yafuatayo "Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yanayojri yote huko Uvinza ...tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupingwa risasi na polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye Matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi:"

Soma zaidi: Ushahidi kesi ya Zitto kuanza kutolewa Januari 29



Chanzo: mwananchi.co.tz