Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi akwamisha kesi ya vigogo wa Simba, Hakimu atoa msimamo

61113 Pic+aveva

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kusikiliza ushahidi katika kesi ya kughushi nyaraka na kutakatisha fedha, inayowakabili vigogo watatu wa klabu ya Simba.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea leo Jumatatu Juni 3, 2019 , baada ya shahidi aliyetakiwa kuja kutoa ushahidi kufiwa na mama mkwe wake.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa rais wa Klabu ya Simba,  Evans Aveva,  makamu wake,  Geofrey Nyange maarufu Kaburu na Mwenyekiti wa  Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai, ameeleza hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Swai amedai  shahidi ambaye walitarajia kuja kutoa ushahidi amefiwa na mama mkwe wake hivyo ameshindwa kufika mahakama kwa ajili ya kutoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.

" Kesi imekuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, lakini nimepewa taarifa na shahidi ambaye alipaswa kuja kutoa ushahidi hapa mahakamani kuwa amepata msiba, amefiwa na mama mkwe wake, hivyo kutokana na hali hiyo tunaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi," amedai Swai.

Pia Soma

Swai baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha tarehe ijayo wanakuja na mashahidi watatu ili kufidia siku ambazo kesi hiyo haijaendelea.

" Tulikubaliana upande wa mashtaka mlete mashahidi wa kutosha, sasa tarehe ijayo nataka mlete mashahidi wa kutosha ili kesi hii iweze kuisha, kwa sababu ni kesi ya muda mrefu," amesema Hakimu Simba.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi, Juni 12 na 13, 2019, kesi hiyo itakapoendelea na ushahidi.

Mshtakiwa  Aveva na Nyange wao wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya utakatishaji fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana huku Hans Poppe, yeye yupo nje kwa dhamana.

Tayari shahidi wanne wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi dhidi ya washitakiwa hao.

Katika kesi hiyo Hans Poppe anakabiliwa na mashitaka mawili, ya kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uongo pamoja na wenzake.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka nane, ambayo ni matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha  bila mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kujipatia fedha isivyo halali (Aveva) na utakatishaji fedha.

Katika maelezo ya awali, washtakiwa hao wanadaiwa  Machi 12, 2016,  Klabu ya Simba ililipwa jumla ya Dola za kimarekani 319, 212 na Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia.

Kiasi  hicho cha fedha kilikuwa ni ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kwenda Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya Tunisia.

Katika shtaka la utakatishaji fedha linalomkabili Aveva, inadaiwa Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays Mikocheni, Dar es Salaam alijipatia Dola za Kimarekani 187,817 kutoka katika Timu ya Simba wakati akijua zimetokana na zao la kosa la kughushi.

Katika shitaka la kughushi linawakabili washtakiwa wote,  wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh. 90Milioni,  huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika shtaka lingine, linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa kati ya March10 na Septemba 30, 2016, waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

Chanzo: mwananchi.co.tz