Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi akwamisha kesi wafuasi Chadema

RUNGU Walikamatwa Agosti 15, 2021 katika kanisa katoliki Kawekamo

Wed, 18 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesi inayowakabili wafuasi 19 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA ya kufanya fujo kanisani Jijini Mwanza, imeendelea kupigwa kalenda baada ya mshtakiwa namba nne kati yao kutokufika mahakamani.

Wafuasi hao wanakabiliwa na kesi namba 77 ya mwaka 2021, baada ya kukamatwa Agosti 15, mwaka jana katika Kanisa Katoliki la Kawekamo Jimbo Kuu la Mwanza. 

Kutokana na mshtakiwa huyo kutofika mahakamani, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Bonaventure Lema aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 1, mwaka huu. 

Hakimu Lema alisema jana ilikuwa siku ya kuanza kupeleka mashahidi wa upande wa Jamhuri baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika mwezi uliopita. 

Wanachama hao Aprili 13, mwaka huu walisomewa maelezo ya awali ya kesi yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza na kukana, huku upande wa mashtaka ukiahidi kupeleka mashahidi saba wakiwamo viongozi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kawekamo Jimbo Kuu la Mwanza na vielelezo vinne vya ushahidi. 

Kesi hiyo ilifunguliwa Agosti 19, 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Mwanza. 

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kufanya ghasia katika mkutano wa dini uliofanyika katika kanisa hilo Agosti 15, mwaka 2021 na kusababisha waumini washindwe kusikiliza neno la Mungu. 

Wanachama hao pamoja na viongozi wa mikoa na kanda kwa pamoja walikana mashtaka hayo mnamo Agosti 19 mwaka jana. 

Makada hao wa Chadema inadaiwa walifika kanisani hapo kwa ajili ya kumuombea mwenyekiti wao wa taifa, Freeman Mbowe ambaye alikuwa mahabusu kwa kesi ya ugaidi.

Wafuasi hao ambao wapo nje kwa dhamana tangu mwaka jana, jana walifika tena katika mahakama hiyo kwa ajili ya kusikiliza ushahidi wa shauri.Washtakiwa hao wanatetewa na wakili Erick Muta na kesi yao imepangwa kuendelea Juni 1, mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza ushahidi upande wa Jamhuri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live