Kesi ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha haramu na kumiliki genge la uhalifu inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (35) na wenzake sita imeahirishwa hadi Machi 14 mwaka huu.
Hakimu Mkazi, Pamela Meela alisema mahakamani jana kuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda anayesikiliza kesi hiyo ana majukumu mengine ya kiofisi nje ya Jiji la Arusha.
Hakimu Meela aliwataka mawakili wa upande wa utetezi na waendesha mashitaka wa serikali wajipange ili Machi 14 kesi hiyo iendelee kwa kuwa Hakimu Kisinda atakuwa amerudi.
Juzi shahidi wa tano, Jackson Macha (30) alidai kuwa hajawahi kupokea mgao wa Sh milioni 1.4 kutoka kwa Sabaya zinazodaiwa kuwa sehemu ya fedha za rushwa ya Sh milioni 90. Mshitakiwa huyo wa sita kwenye kesi hiyo alisema hayo wakati akiongozwa na Wakili Edmund Ngemela.
Alidai kuwa hakuhusika na mgao wa Sh milioni 1.4 uliodaiwa kutolewa na Sabaya katika Hoteli ya Tulia ya jijini Arusha kwa kuwa hakuwahi kuomba wala kushawishi rushwa ya kiasi hicho wala kupokea fedha hizo.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Enock Mnkeni (41), Watson Mwahomange (27), John Aweyo (45), Syliverster Nyegu (26) na Nathan Msuya (31).