Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi afunguka alivyobadilishana nguo na mtuhumiwa kesi ya mauaji

Msuya Bilionea.jpeg Shahidi afunguka alivyobadilishana nguo na mtuhumiwa kesi ya mauaji

Wed, 23 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika mwendelezo wa usikilizwaji wa kesi ya mauaji ya Aneth Msuya leo Jumanne, Agosti 22,2023, shahidi ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam namna alivyoshiriki katika gwaride la utambuzi wa mshtakiwa wa pili katika kesi ya mauaji hayo.

Shahidi huyo wa 20, Nassib Adrian (47) mkazi wa Njiro Arusha aliieleza mahakama kuwa, mshtakiwa huyo Revocatus Everist Muyella alisimama pembeni yake kwamba alibadilishana naye nguo za juu (fulana na shati) kisha shahidi mtambuzi alipopita alimtambua mshtakiwa huyo.

Aneth ambaye aliuawa Mei 25, 2016 nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, alikuwa mdogo wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya

Washtakiwa katika kesi hiyo Miriam Steven Mrita, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na mjane Bilionea Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mjohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013; pamoja na Revocatus Everist Muyella (mshtakiwa wa pili).

Kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018 inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, na washtakiwa wote wanakabiliwa na shtaka moja tu la mauaji hayo.

Kwa mujibu wa ushahidi wake, akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Marietha Maguta, wakati huo mwaka 2016 alikuwa anaishi Keko Dar es Salaam akijishughulisha na biashara ya kuuza chips anayoifanya mpaka sasa huko Arusha.

Siku ya tukio Agosti 21, 2016 alifika katika kituo cha Polisi Kilwa Road, kumfuatilia mtoto wa dada yake aliyekuwa amekamatwa ndipo akaombwa na askari mmoja kushiriki katika gwaride la utambuzi wa mshtakiwa huyo.

Alikubali yule askari alimwelekeza akazunguka nyuma ya kituo hicho ambako aliwakuta watu wengine wanne na baadaye wakaongezeka wengine wakafika wanane, na wote walikuwa wanalingana urefu na kufanana rangi.

Msimamizi wa gwaride aliwalekeza wasimame mstari mmoja, kisha askari mwingine wa kiume alimleta mtuhumiwa akamweleza kuwa anaweza kuchagua sehemu yoyote ya kusimama na kwamba anayo haki hata ya kubadilishana mavazi na watu wengine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live