Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aelezea kesi ya mwalimu kubaka, kulawiti mwanafunzi

18356 MWALIM+PIC TanzaniaWeb

Fri, 21 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Shahidi wa tatu katika kesi ya kubaka na kumlawiti mwanafunzi inayomkabili mwalimu wa Shule ya Sekondari Adili, Joel Mbaga (27), leo Septemba 20, 2018 ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arusha kuwa alipata taarifa za tukio hilo baada mwanafunzi huyo kutoonekana shuleni.

Shahidi huyo, Florian Masawe ambaye ni mwalimu katika shule hiyo amesema baada ya mwanafunzi kutoonekana shuleni, mama wa mwanafunzi aliyetendewa kitendo hicho, Agness Augustino alimpa taarifa ya tuhuma za mwalimu mwenzake kwamba amekuwa akimbaka mwanae.

Amesema awali alipokea barua ya mwanafunzi huyo kuwa hataki kurejea shuleni kutokana na kuingiliwa na popobawa usiku akiwa amelala shuleni.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Naomi Mollel, shahidi huyo alieleza kumtambua mwalimu Mbaga ambaye alikuwa ndio mwalimu wa malezi katika shule hiyo.

Amesema kwa mujibu wa taratibu za shule, Mbaga ndio alikuwa akifuatilia taratibu zote za kulala wanafunzi shuleni na kama kuna tatizo yeye ndio hutoa taarifa kwa uongozi wa shule.

Hata hivyo, amesema mwalimu Mbaga hakuwahi kutoa taarifa juu ya tukio la mwanafunzi huyo kuingiliwa na popobawa kama ambavyo mwanafunzi aliandika katika barua yake ya awali.

Amesema Oktoba mwaka jana, wakati uongozi wa shule ukifuatilia suala hilo, polisi walifika na kumkamata mwalimu Mbaga.

Katika kesi hiyo namba 165 ya mwaka 2018, inayosikilizwa na hakimu mkazi, Patricia Kisinda, upande wa mashtaka unatarajia kuita mashahidi watano ambapo mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Septemba na Oktoba, 2017.

Kabla ya shahidi huyo wa tatu, mashahidi wengine waliotoa ushahidi wao, ni mwanafunzi aliyetendewa kitendo hicho na shahidi wa pili alikuwa ni mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Agness Augustino.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 8, 2018 huku mwalimu huyo akiwa nje kwa dhamana.

Chanzo: mwananchi.co.tz