Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aeleza yaliyojiri kabla ya ‘house girl’ wa Jaji kuuawa

45015 Pic+shahidi Shahidi aeleza yaliyojiri kabla ya ‘house girl’ wa Jaji kuuawa

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Saa chache kabla ya kuuawa kwa aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa kike ‘house girl’ wa Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Engera Kileo, marehemu Lucy Pepetua Maina;  mshtakiwa, Philemon Zakaria Laizer, pamoja na wanafamilia wengine walishiriki chakula na ibada ya usiku kwa pamoja.

Hayo yamebainishwa na shahidi wa sita wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo, Heri Goitiama wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Yose Mlyambina katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam. Katika kesi hiyo  ya jinai namba 96, Philemon anadaiwa kumuua  Lucy Juni 8, 2013 usiku.

Philemon ambaye ni mwenyeji wa Arusha na Lucy ambaye alikuwa raia wa Kenya walikuwa wafanyakazi wa nyumbani kwa Jaji Kileo.

Mwili wa Lucy uliokotwa asubuhi ya siku hiyo ya tukio ukiwa umetelekezwa kichakani karibu na jalala, mita chake kutoka nyumbani kwa Jaji Kileo, eneo la Mikocheni B, katika nyumba za makazi ya viongozi wa Serikali.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Anna Chimpaye, Goitiama ambaye alikuwa mmoja wa wanafamilia wa Jaji Kileo, amesema alikuwa na kawaida ya kumfundisha Lucy namna ya kutumia kompyuta kabla ya kulala.

Shahidi huyo alidai siku hiyo ya tukio, Ijumaa ya Juni 7, 2013, wanafamilia wote, akiwemo marehemu na mshtakiwa walishiriki chakula cha jioni na baada ya chakula walishiriki wote sala ya usiku kabla ya kwenda kulala.

Alidai wakati wengine walipoingia vyumbani mwao kulala, yeye alibaki na marehemu akiendelea kumfundisha kompyuta kama ilivyokuwa kawaida na kwamba baada ya muda yeye naye alikwenda kulala na akamwacha marehemu akiendelea kujifunza mwenyewe.

Goitiama alisema Lucy alikuwa na kawaida ya kuwahi kuamka mapema asubuhi lakini siku hiyo, Juni 8, 2013 mpaka saa sita mchana alikuwa hajaonekana.

“Mimi na Philimon (mshtakiwa) tulikwenda chumbani kwake na sehemu nyingine za nyumba lakini hakuonekana, chumbani kwake tulikuta kitanda tu na mabegi yake hayakuwemo.”

“Nilijaribu kumpigia simu Lucy ili kufahamu alikuwa yuko wapi lakini hakupatikana.”, alisema shahidi Goitiama.

Alieleza baadaye walipata taarifa kuna askari walionekana eneo lile na kwamba kuna mwili wa mtu ulikuwa umeokotwa, ndipo wakaenda mpaka kwa wale askari nao wakawaeleza kuna mwili wa msichana uliokotwa na kwamba ulikuwa umepelekwa Hospitali ya Mwananyamala.

Hivyo alisema waliwataka kwenda kuuangalia kama wanaweza kuutambua, walipofika waliutambua ulikuwa ni wa Lucy na kisha wakaenda kutoa taarifa kituo cha polisi Oysterbay kuwa wameutambua, ambapo waliandika maelezo yao kisha wakarudi nyumbani.

Hata hivyo, alipoulizwa na wakili wa mshtakiwa, Nehemia Nkoko, iwapo wakati huo walipokuwa wakimtafuta Lucy baada ya kutoonekana nyumbani, mshtakiwa alionekana kuwa na mashaka au kustuka, alijibu kuwa hakuonesha mshtuko wala mashaka.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz