Shahidi wa nne katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu ameeleza namna alivyoshuhudia mshitakiwa wa pili na wa tatu wakikamatwa na kupekuliwa katika eneo la Rau Madukani mjini Moshi.
Katika kesi hiyo mshitakiwa wa pili ni Adam Kasekwa na wa tatu ni Mohammed Ling'wenya.
Shahidi huyo Anitha Valerian ambaye ni mfanyabiashara wa mbege katika eneo hilo alitoa ushahidi jana katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Mbele ya Jaji Joachim Tiganga, Anitha alidai kuwa Agosti 5 mwaka jana saa saba kasoro mchana alitoka saluni kwenda kufanya usafi katika eneo lake la biashara na alipita katika moja ya maduka akaona vijana wawili waliokuwa wakinywa bia na kusajili laini za simu.
Alidai kuwa akiwa ofisini kwake alishuhudia vijana hao (Kasekwa na Ling'wenya) wakipitapita na kuongea na simu na baada ya muda mfupi waliwekwa chini ya ulinzi.
"Walikuwa ni maaskari, waliwaambia mko chini ya ulinzi kwa sababu mnahusika na mambo ya kigaidi," alidai Anitha. Alidai kuwa vijana hao walitekeleza amri ya kukaa chini na hali ya eneo husika ilikuwa shwari na hakukuwa na purukushani yoyote.
Anitha alidai kuwa wakati vijana hao wakiwa hapo walikwenda askari wengine watatu hivyo wakawa askari watano na mmoja wao alijitambulisha kwa jina la Jumanne.
Alidai kuwa Jumanne aliwaeleza Kasekwa na Ling'wenya kuwa alihitaji kuwapekua lakini kabla ya kufanya hivyo alijipekua na kuwahakikishia kuwa hakuwa amebeba kitu chochote.
Alidai baada ya kujipekua alimsimamisha mmoja wa kati ya watuhumiwa ambaye baada ya kuulizwa jina alijitambulisha kwa jina la Adam Kasekwa.
Anitha alidai kuwa, wakati akipekuliwa Kasekwa alidaiwa kukutwa na bastola, simu ndogo aina ya Itel na kete ndogo zilizodhaniwa zilikuwa dawa za kulevya.
Alidai kuwa katika upekuzi huo Ling'wenya alikutwa na kete ndogo 26 zilizodhaniwa ni dawa za kulevya na simu aina ya Tecno nyeusi iliyokuwa na laini za mitandao ya Halotel na Airtel.
Anitha aliomba kuwasilisha hati ya maelezo aliyoyatoa ili yawe sehemu ya kielelezo katika shauri hilo. Maelezo hayo yalipokelewa kama kielelezo namba D1.