Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aeleza viwanja anavyomiliki Gugai

66043 Gugai+pic

Tue, 9 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ofisa  ardhi mteule kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Anicas  Vilumba (40) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliyekuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai anamiliki viwanja viwili katika manispaa hiyo.

Vilumba ambaye ni shahidi wa 17  katika kesi ya utakatishaji wa fedha inayomkabili Gugai na wenzake watatu, ameieleza mahakama hiyo jana Jumatatu Julai 8, 2019 wakati akitoa  ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.

Akiongozwa na wakili wa Serikali  mwandamizi, Awamu Mbagwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, shahidi huyo  amedai  hati za viwanja hivyo zipo katika kumbukumbu za majalada yaliyopo katika ofisi ya Halmashauri ya Manispaa hiyo.

" Moja ya makujumu yangu ni kutunza kumbukumbu za majalada yanayotokana na ardhi, kusaini nyaraka za umiliki wa ardhi na mabadiliko ya ardhi, pia mimi ni mkusanyaji mkuu  wa maduhuli,” amedai  Vilumba ambaye ameajiriwa kuwa Ofisa Ardhi Mteule katika Halmashauri hiyo tangu 2017.

Shahidi huyo amevitaja viwanja viwili, anavyomiliki Gugai kuwa ni  kiwanja namba 126, kitalu A na Kiwanja namba  29, kitalu L, vyote vipo katika Halmashauri  hiyo.

"Mmiliki wa viwanja hivyo mpaka sasa ni Godfrey Gugai, ambaye kiwanja namba 126, alianza kukimiliki  tangu  mwaka 2011 huku kiwanja namba 29, alikimiliki tangu  mwaka 2012 hadi sasa" amedai Vilumba.

Pia Soma

Shahidi huyo aliiomba Mahakama hiyo ipokee hati mbili za viwanja  anavyomiliki Gugai, kama sehemu ya ushahidi mahakamani hapo.

"Naomba kutoa majalada haya mawili ambayo ni hati za viwanja za Gugai anazomiliki katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, yatumike kama ushahidi Mahakamani hapa" amedai Vilumba.

Mahakama hiyo imepokea hati hizo kama vielelezo vitakavyotumika katika kesi hiyo.

Shahidi baada ya kutoa ushahidi wake, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi kesho itakapoendelea na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Tayari mashahidi 17 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Miongoni mwa mashahidi hayo ni Msajili wa Hati Msaidizi, kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Joanitha Kazinja.

Katika ushahidi wake Kazinja, alidai Mahakama hapo kuwa Gugai anamiliki hati nane za viwanja katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Kazinja alidia kuwa hati hizo ni moja ya mali anazotuhumiwa kumiliki Gugai na kwamba mshtakiwa huyo ni mmoja wa wamiliki walioandikishwa katika kumbukumbu za hati za ardhi, ambao wamesajiliwa na wizara ya Ardhi.

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo  ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, linamkabili Gugai.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo anadaiwa kutenda  kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba, 2015.

Inadaiwa kuwa akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru, Gugai anadaiwa kumiliki mali za zaidi ya Sh 3.6 bilioni ambazo hazilingani na kipato chake cha awali na cha sasa, huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Chanzo: mwananchi.co.tz