Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aeleza polisi walivyomnyang’anya mshtakiwa begi

Hukumu Pc Data Shahidi aeleza polisi walivyomnyang’anya mshtakiwa begi

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa sita wa upande wa mashtaka katika kesi ya kusafirisha meno ya tembo yenye thamani ya Sh34 milioni, inayomkabili Abubakari Msawa (41) maarufu kama Ustaadh, ameieleza Mahakama jinsi alivyoshuhudia mshtakiwa huyo akinyang'anyana begi lililokuwa na meno ya tembo na askari Polisi.

Shahidi huyo, Waziri Hamidu (39), mkazi wa Mahenge mkoani Morogoro ametoa maelezo hayo leo, Februari 28, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi, wakati akitoa ushahidi wake.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Judith Kyamba akisaidiana na Titus Aaron, Hamidu amedai Juni 21, 2018, alikuwa kwenye biashara yake ya umachinga anayoifanya katika eneo hilo.

"Baada ya kurudi kutoka katika biashara yangu, nilikwenda dukani jirani na ninapoishi na nikiwa eneo hilo, saa moja usiku nilisikia kelele kama watu wanagombana," amedai.

Amebainisha wakiwa njiani kwenda eneo hilo, waliona watu wawili wakiendelea kugombana na wao walihisi huenda ni mwizi anapigwa.

"Tulipokuwa tunakaribia eneo hilo, tuliona watu wawili wanatoka kwenye uchochoro wa nyumba na ghafla mmoja alijitambulisha kuwa ni askari Polisi na wamekuja eneo hilo kwa ajili ya ukamataji.

“Mimi na wenzangu tulisimama tu kuangalia jinsi walivyokuwa wakinyang'anyana begi hilo," amedai.

Ameeleza baada ya askari kufanikiwa kumkamata na kumnyang'a begi hilo rangi nyeusi, walimuamuru alifungue na walikuta vipande vitatu vya meno ya tembo, suruali moja rangi kijivu pamoja na shati moja lenye mistari rangi nyeupe na nyeusi.

Amedai baada ya kutoa vitu hivyo, askari moja aitwaye Beatus alitoa hati ya ukamataji na kuanza kuviorodhesha vitu hivyo katika fomu hiyo.

" Beatus aliniuliza majina yangu na kuandika maelezo yangu kwa ufupi na kunitaka niweke saini katika hati hiyo na kunieleza kuwa ikitokea wananihitaji, basi watanipigia simu" amedai Hamidu.

Baada ya Hamidu kumaliza kutoa ushahidi, aliulizwa maswali na mshtakiwa na miongini mwa maswali hayo ni kama yafuatayo;

Mshtakiwa: Elimu yako ndugu shahidi.

Shahidi: Darasa la saba.

Mshtakiwa: Unaelewa tofauti kati ya shati ya t-shirt? Maana wakati unatoa ushahidi umesema ndani ya begi walikuta tisheti na suruali! Usahihi ni upi hapo?

Shahidi: Nilisema ndani ya begi, kulikutwa suruali moja na shati na sio tisheti.

Mshtakiwa: Ulishafanya kazi Maliasili?

Shahidi: Hapana.

Mshtakiwa: Sasa je, kama hayo ni meno ya ng'ombe na sio ya tembo, wewe umeyatambuaje wakati hufanyi kazi Maliasili?

Shahidi: Nayajua meno ya tembo na meno ya ng'ombe.

Shahidi: Sisi tuliobahatika kuishi porini tunajua meno ya tembo yakoje na meno ya ng'ombe yakoje, kwa hiyo haya yaliyoletwa hapa mahakamani ni meno ya tembo?

Shahidi baada ya kumaliza kuulizwa maswali na mshtakiwa, hakimu Msumi aliahirisha kesi hadi Machi 12, 2024 itakapoendelea na ushahidi na mshtakiwa alirudishwa rumande.

Katika kesi ya msingi, Msawa ambaye ni kondakta wa magari, anadaiwa Juni 21, 2018 eneo la Kiwalani Wilaya ya Ilala alikutwa na vipande vitatu vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh34 milioni, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live