Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aeleza mke wa bilionea Msuya alivyopanga mauaji ya wifiye

Mke Wa Msuya Shahidi aeleza mke wa bilionea Msuya alivyopanga mauaji ya wifiye

Thu, 24 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, WP Sajenti Mwajuma katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya, amedai mahakamani kuwa, mshtakiwa wa kwanza Miriam Mrita alikiri kupanga njama za mauaji hayo ya wifi yake.

Akitoa maelezo ya awali katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana, Sajenti Mwajuma aliyemhoji mshtakiwa huyo, alidai kuwa Miriam alikiri kuhusika na mauaji hayo kwa madai kuwa, wifi yake alikuwa akimfuata fuata sana.

Akizungumza namna Miriam alivyopanga mauaji hayo, Sajenti Mwajuma alidai kuwa, awali mshtakiwa aliteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu mumewe, bilionea Erasto Msuya aliyeacha wosia kuwa, asilimia 40 ya fedha alizoacha benki wapewe wazazi na dada zake na asilimia 60 iliyobaki apewe mkewe pamoja na watoto wake.

Sajenti Mwajuma alidai kuwa, marehemu Bilionea Msuya katika wosia huo alieleza kuwa mali zingine yakiwamo magari, mgodi na hoteli zinapaswa kugawanywa kwa utaratibu wa mirathi.

Shahidi huyo alidai kuwa, kwa mujibu wa Miriam alifungua shauri la mirathi katika Mahakama Kuu Arusha kwa kumtumia wakili aliyechaguliwa na familia.

Alidai kuwa, baadaye Miriam aliliondoa shauri hilo mahakamani bila ya kumweleza wakili aliyechaguliwa na familia sababu ya kufuta shauri hilo na kutafuta wakili mwingine bila ya kukaa kikao.

Shahidi alidai kuwa wakati akimhojiwa, Miriam alidai kugawa fedha hizo za benki bila ya kuwa na mgogoro wowote, huku akisema asilimia 40 ilienda kwa wazazi na ndugu wa marehemu na asilimia 60 ilienda kwake na kwa watoto.

Shahidi alidai kuwa, baadhi ya mali za marehemu, mshtakiwa huyo alizorodhesha kwa jina lake kitendo kilichosababisha kutokuwa na maelewano mazuri na ndugu wa marehemu mume wake.

“Mshtakiwa huyo alipata taarifa kuwa kuna ndugu wa marehemu mume wake Dar es Salaam walipigwa risasi walikuwa wamelazwa lakini hakuwahi kuonana nao kwa sababu hawakuwa na mahusiano mazuri,” alidai shahidi huyo.

Sajenti Mwajuma alidai kuwa, baada ya tukio hilo la kupigwa risasi dada wa marehemu Bilionea Msuya, ndipo likafuatia tukio la mauaji ya Aneth.

Akizungumza mahakamani hapo, shahidi alidai kuwa Miriam alikiri kuwa ndiye aliyehusika na mauaji hayo baada ya ya kuona kuwa Aneth alikuwa anamfuata fuata sana.

Akielezea mpango wa kutekeleza mauaji hayo wakati akihojiwa, Mrita alisema alimpa kazi hiyo mtu anayeitwa Ray kwa makubaliano ya malipo ya Sh20 milioni.

Shahidi alidai kuwa, Miriam alimpigia simu Ray na kumuuliza kama anafahamu anapoishi Aneth, alimjibu anajua anaishi Kibada.

Shahidi alidai kuwa, Miriam alisema Mei 15,2016, Ray alimpitia yeye na wakaelekea Kibada, Kigamboni wakiwa na gari lao aina ya Range Rover ili kutafuta nyumba aliyokuwa anaishi Aneth na walipofika eneo hilo walikutana na binti wa kazi wa Aneth.

“(Ray na Mriam) walimuuliza binti huyo kama anapajua nyumbani kwa Aneth, akawajibu ni pale na yeye anaishi kwenye nyumba hiyo,” alidai shahidi mahakamani hapo.

“Walimuuliza binti huyo kama ana simu akawajibu hana, hivyo walimuahidi kumnunulia na wakakubaliana kuwa Mei 18, 2016 na wamkute nje ya nyumba hiyo. Mei 18 walikwenda na kumkuta binti huyo nje ya nyumba hiyo kama walivyokuwa wamekubaliana, hivyo wakampatia simu kwa ajili ya mawasiliano binafsi,” alidai shahidi huyo.

“Wakati huo Ray alikuwa amebeba ‘briefcase’ nyeusi ndani kulikuwa na Sh10 milioni, lengo lao kumuonyesha binti huyo (msichana wa kazi) akubali ombi lao ili siku ya tukio, asiwepo nyumbani badala yake alitakiwa kuondoka,” alidai shahidi huyo.

“Mei 23,2016 asubuhi Miriam alimpitia Ray pamoja na jamaa zake Magomeni kwa ajili ya kazi hiyo na ilipofika Mei 25, 2016, Miriam alipelekwa mkoani Arusha. Mei 26,2016 Miriam akiwa Arusha alipata taarifa kwamba Aneth ameuawa kwa kuchinjwa na yeye, lakini hakwenda kwenye mazishi kwa sababu mama mkwe wake alikuwa amemwambia kuwa ikitokea yeye amekufa au familia ya mume wake asiende kwenye mazishi.

“Mei 27, 2016 Ray alisafiri na kuelekea Arusha hadi kwenye hoteli ya mshtakiwa huyo ili akamaliziwe fedha zake zilizobaki Sh10 milioni ambazo alipewa,” alidai shahihi huyo.

Baada ya kumaliza kusoma maelezo ya mshtakiwa huyo, shahidi huyo wa kwanza alieleza kuwa, baada ya mshtakiwa huyo kukamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Chang’ombe Agosti 7,2016 alifanyiwa gwaride la utambuzi.

Pingamizi latupwa

Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu imetupilia mbali pingamizi la mshtakiwa wa kwanza, Miriam katika kesi hiyo kuhusu kupokewa kwa maelezo yake ya ungamo aliyoyatoa mbele ya shahidi wa pili wa upande wa mashtaka, Mlinzi wa Amani.

Badala yale Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Edwin Kakolaki imekubaliana na hoja za upande wa mashtaka na kuyapokea maelezo hayo ya ungano kuwa kielelezo cha pili cha upande wa mashtaka.

Jaji Kakolaki alisema ili kitu chochote kipokewe mahakamani kuwa kielelezo, lazima kitimize masharti matatu.

Alisema kwanza ni nyaraka, iwe halisi na kama ni nakala kivuli ina utaratibu wake. Pili ni uhusiano na shauri husika na sharti la tatu ni mamlaka kwa mtoaji.

Jaji Kakolaki alisema vigezo hivyo vyote vimetimia na Mahakama ilipokea maelezo ya ungamo ya mshtakiwa Miriam Agosti 10, 2016 kuwa kielelezo cha pili cha upande wa mashtaka.

Awali, upande wa utetezi katika kesi hiyo unaotetewa na

Wakili Peter Kibatala ulipinga kupokewa maelezo ya ungamo kwa sababu shahidi aliyechukua maelezo hayo kuwa alitoka Wilaya ya Ilala wakati mshtakiwa Miriam alikamatwa na kuhojiwa Wilaya ya Temeke.

Kibatala alidai katika utambulisho wa shahidi huyo alijitambulisha kama hakimu mstaafu wa Mahakama ya Mwanzo Ilala na kumbukumbu zinaonyesha, mshtakiwa alikamatwa na kuhojiwa Temeke.

“Kuna kifungu kinasema mtu atafanyiwa maungamo katika Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya alikokamatiwa na si wilaya nyingine tumeona mshtakiwa amekamatwa na kuhojiwa Wilaya ya Temeke na shahidi ametoka Wilaya ya Ilala, hivyo mshtakiwa huyu alitakiwa ahojiwe na mlinzi wa amani wa wilaya husika,” alisema Kibatala.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Mwandamizi wa upande wa Jamhuri, Erick Tesha alieleza Mahakama kuwa pingamizi lililotolewa na upande wa utetezi halikuwa na mashiko kwa sababu, shahidi huyo yupo sahihi, alichukua maelezo yake kwenye eneo linaloruhusiwa kisheria kifungu cha 58 cha sheria iliyoanzisha Mahakama ya Wilaya na Mwanzo (MCA).

Tesha alidai kuwa, ingetokea shahidi huyo ametoka Wilaya ya Ilala na kwenda Temeke kuchukua maelezo ya ungamo ndipo kifungu alichosema kingeleta maana kama ilivyowasilishwa.

“Shahidi wangu yupo sahihi kutoa ushahidi kwa kuwa shauri hili lilikuwa linapelelezwa na mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kipolisi Temeke pamoja na mkuu wa upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, hivyo alikuwa sawa kuchukua maelezo ungamo haijalishi ametokea wilaya gani,”alidai Tesha. Baada ya maelezo hayo, Jaji Kakolaki aliahirisha kwa muda kabla ya kurejea na kutupilia mbali pigamizi hilo.

Awali, Mlinzi wa Amani ambaye ni Hakimu mstaafu wa Mahakama ya Mwanzo Ilala akiongozwa na wakili mwandamizi Tesha, alidai Agosti 10, 2016 alikuwa katika Mahakama ya Ilala alimpokea mshtakiwa Miriam ambaye aliletwa na askari Sajenti Mwajuma alimfikisha kwake akituhumiwa na kesi ya mauaji.

Alidai baada ya kumfikisha mshtakiwa huyo alimwambia askari huyo atoke nje yeye akabaki na mshtakiwa pamoja na karani wa mahakama hiyo, kabla ya kuanza kumuhoji mshtakiwa huyo kwa taratibu za kupokea maelezo.

Alidai baada ya kumuuliza kosa analokabiliana nalo, mshtakiwa huyo alikubali kuwa ni yeye alitenda kosa hilo na akaanza kujieleza hadi alipofanya mauaji hayo.

Aliendelea kuieleza Mahakama kuwa wakati wanafanya mahojiano hayo, alikuwa anaandika kisha akimsomea na alikubali kukiri kuwa maelezo aliyoyatoa kuwa ni yake.

Mbali na Miriam, mshtakiwa mwingine ni mfanyabiashara Revocatius Muyella ambaye wanakabiliwa na kesi ya kumuua kwa kukusudia Aneth.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live