Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aeleza mgogoro wa ndoa ulivyompeleka kwa ‘Mfalme Zumaridi’

Zumaridipic Data Shahidi aeleza mgogoro wa ndoa ulivyompeleka kwa ‘Mfalme Zumaridi’

Fri, 19 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Shahidi katika kesi inayomkabili Diana Bundala, maarufu kama ‘Mfalme Zumaridi’ ameieleza mahakama kuwa mgogoro wa ndoa na mzazi mwenzake ndio ulimfanya kuondoka na mtoto wao na kukimbilia kwenye kanisa la mshtakiwa huyo.

Ally Shaaban aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mwanza, leo Ijumaa Agosti 19, 2022 kuwa mgogoro na mzazi mwenzake, Suzana Simon kulitokana na kupungua kwa upendo kati yao, jambo lililosababisha kupungua kwa mvuto wa mahusiano kati yao.

Akiongozwa na wakili wa utetezi, Erick Mutta, Shaaban ameeleza kuwa Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni ilitoa amri mbili za kufuata kabla ya kumchukua mtoto wao kwa mama yake.

Alidai mahakama hiyo ilimwamuru kuhakikisha anaihudumia familia hiyo na kumruhusu mkewe aondoke iwapo hawataelewana na ndiyo maana aliamua kufungua kesi ya kutaka aruhusiwe kumchukua mtoto huyo.

Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Monica Ndyekobora ameuagiza upande wa mashtaka kubainisha idadi ya mashahidi watakaowatumia.

Washtakiwa wengine katika kesi ni Amos Abdul, Isaya John, Isack Mashaka, Neema Julian, Suzan Simon, Anita Isaya, George Maloji na Veronica Mgaya.

Advertisement Wanashtakiwa kwa kufanya shambulio la kudhuru mwili wanalodaiwa kulitenda Februari 26, 2022 huko Buguku jijini Mwanza.

Leo shahidi wa nane, tisa pamoja na Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Nyamagana Sajenti Robert (49) wametoa ushahidi wao wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Dorcas Akyoo na Mwanahawa Changale.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wao Hakimu, Monica Ndyekobora ameliagiza jopo la mawakili wa Serikali kuchambua na kuwasilisha idadi halisi ya mashahidi katika kesi hiyo kwa kile alichoeleza kuhakikisha kesi hiyo inamalizika ndani ya muda uliopangwa.

"Upande wa mashtaka chambueni mashahidi wenu tujue wamebakia wangapi kwa sababu kuna muda maalum shauri kuendeshwa ili haki itendeke kwa mshtakiwa na jamhuri," amesema Ndyekobora.

Hata hivyo, Wakili Akyoo amesema Agosti 31, 2022 shauri hilo litakapotajwa upande huo utakuja na idadi kamili ya mashahidi wao.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 31, 2022 itakapotajwa tena

Sehemu ya mahojiano kati ya mawakili na shahidi yalikuwa kama ifuatavyo

Mutta: Shahidi tukumbushe dini yako?

Shahidi: Muislamu

Mutta: Umewahi kupata elimu ya dini?

Shahidi: Ndiyo madrasa

Mutta: Unaufahamu Uislamu vizuri?

Shahidi: ndiyo

Unaweza kufunga kifua chako kwa kuwa imani yako hairuhusu?

Shahidi: (Anafunga)

Mutta: Uliwahi kumuuliza mama mtoto wako kwa nini anang'ang'ania mtoto wake?

Shahidi: Sikumbuki

Mutta: Unatambua kwamba mtoto aliishi tumboni kwa mama yake hakuwahi kuishi na baba yake?

Shahidi: Ndiyo

Mutta: Unafahamu anayejua baba halali wa mtoto ni mama?

Shahidi; Ndiyo

Mutta: Umewahi kuhoji uhalali ni nani baba wa mtoto?

Shahidi: Ndiyo, alisema ni mtoto wangu

Mutta: Unafahamu mapenzi ya mtoto kwa mama na kwa baba?

Shahidi: Sielewi

Mutta: Unafahamu mwaka 2021 wakati wa migogoro huo mliwahi kubishania ni wapi mtoto akasome?

Shahidi: Ndiyo nakumbuka

Mutta: Unakumbuka mama wa mtoto alisema ana uwezo wa kumsomesha mtoto huyo?

Shahidi: Hana uwezo huo

Mutta: Unafahamu wewe na mama wa mtoto wako mapenzi yaliisha?

Shahidi; Ni kweli yaliisha

Mutta: Mtoto anazungumza, ni lini alikwambia amechoka kuishi na mama yake, achilia amri ya mahakama?

Shahidi: Sikumbuki

Mutta: Ulifanya jitihada zozote za kumtafutia nyumba ya kuishi?

Shahidi: Ndiyo nilifanya

Mutta: Upo wapi uthibitisho?

Shahidi: Zipo karatasi ila sikumbuki zilipo

Mutta: Una uthibitisho wowote wa jitihada za kutaka kumtunza mtoto na mama kama ilivyokuwa imeamriwa?

Shahidi: Sikumbuki

Mutta: Katika mambo yaliyoamriwa hayo niliyoyataja, kuchukua mtoto lilikuwa jambo la mwisho?

Shahidi: Sikumbuki

Mutta: Unafikiri kwa nini mahakama ilikuamuru umtunze na yeye achukue vitu vyote?

Shahidi: Kwa sababu mimi ni mzazi mwenzie

Mutta: Dini ni utashi binafsi? Hakuna mtu anayempangia mwenzake dini na imani ya kuabudu?

Shahidi: Ni kweli

Mutta: Unakubaliana na mimi kwamba hakukuwa na makwazo yoyote pale mtu anapochagua imani na dini ya kuabudu?

Shahidi: Kweli

Mutta: Unakumbuka kwamba hakukuwa na makubaliano ya dini ya kuamini?

Shahidi: Makubaliano yetu ilikuwa abadili dini ila sikumbuki yalipo makubaliano hayo.

Mutta: Una kumbukumbu yoyote juu ya haya yanayoendelea hapa mahakamani?

Shahidi: Sikumbuki

Mutta: Tarehe 25, 2022 wewe na Wakili wako ambaye hujamtaja na ndugu yako mlienda kituo cha polisi kupeleka nyaraka hizo?

Shahidi: Siyo kweli

Mutta: Ikiwa watu wawili wanaongea mambo mawili tofauti kwenye jambo moja, Unakubaliana na mimi kwamba kuna mmoja ni muongo?

Shahidi: Inawezekana

Mutta: Ndani ya gari ya polisi ulikaa nyuma au mbele?

Shahidi: Wakati tunaenda nilikaa mbele

Mutta: Nani na nani walikaa mbele?

Shahidi: Watatu

Mutta: Katika hao kulikuwa na askari?

Shahidi: Mimi nilipewa askari

Mutta: Afisa Ustawi alikaa wapi!?

Shahidi: Alikaa nyuma

Mutta: Ni wewe peke yako uliyebaki ndani ya gari?

Shahidi: Sikumbuki

Mutta: Umeieleza Mahakama, ukiwa ndani ya gari ulisikia sauti mahali Polisi walipoelekea, ni kweli?

Shahidi: Ni kweli

Mutta: Tueleze kama umewahi kupata tatizo la macho la kutoona vizuri?

Shahidi: Sikumbuki

Mutta: Unakubaliana na mimi mahala Polisi walipoelekea ulikuwa hupaoni ndiyo maana ulikuwa unasikia sauti pekee?

Shahidi; Ni kweli

Mutta: Unafahamu tofauti ya kuanguka na kuangushwa? Kwamba kuanguka ni kutenda na kuangushwa ni kutendewa?

Shahidi: Ni kweli

Mutta: Ili useme ameangushwa ni lazima ushuhudie kwa macho yako?

Shahidi: Ndiyo

Mutta: Unakubaliana na mimi kwamba ulivyoshuka ulikuta Afande James alikuwa amedondoka?

Shahidi: Ndiyo

Mutta: Umeieleza mahakama ukashuka, ulimkuta Afande James amedondoshwa?

Shahidi: Ndiyo

Mutta: Unakubaliana na mimi kwamba ulipokuwepo uliishia kusikia kelele tu, hukuweza kuwaona waliomdondosha bali hukuona waliomdondosha?

Shahidi: Niliona alipodondoshwa

Mutta: Kudondoka kwa mtu au kitu kuna weza kusababishwa na yeye mwenyewe au ukasabanishiwa na watu wengine?

Shahidi: Ni kweli

Mutta: Kudondoka kwa James uliona baada ya kushuka kwenye gari?

Shahidi: Kweli

Mutta: Eneo lile ni mara ya kwanza kufika na huna uzoefu wa sauti ya mtu yoyote?

Shahidi: Kweli

Mutta: Hakuna wakati wowote  iwe Ustawi wa Jamii au Polisi baada ya tukio ulienda kuandika ripoti yoyote juu ya kuchukua mtoto au kutochukua?

Shahidi: Niliiachia Polisi

Mutta: Suzan uliishia kumtambua kwa kumuona?

Shahidi: Kweli

Mutta: Mbali na kumuona na kumtambua hakuna chochote kati yenu kilichotokea?

Shahidi: Tuliishia kutazamana tu

Mutta: Na mtoto hakuwa eneo hilo wala hukumuona?

Shahidi: Sikumuona

Mutta: Baada ya kutomuona mtoto mkaondoka?

Shahidi: Tuliondoka kwa sababu ya fuko zilizopo.

Mutta: Tueleze kuishi maisha ya Zumaridi maana yake ni nini?

Shahidi: Sitambui

Mutta: Na hukuwai kumuuliza mkeo?

Shahidi: ndiyo

Mutta: Mheshimiwa ni hayo tu.

Chanzo: Mwananchi