Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aeleza jinsi aliyekuwa mgombea ubunge ACT Wazalendo alivyoghushi sahihi za nduguze

86206 Pic+sahihi Shahidi aeleza jinsi aliyekuwa mgombea ubunge ACT Wazalendo alivyoghushi sahihi za nduguze

Thu, 28 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam nchini Tanzania, Paskazia Gwaje (33), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  jinsi mwanasiasa Salma Mtambo, alivyowasilisha maombi ya kuhamisha umiliki wa ardhi bila kushirikisha ndugu zake.

Pia, anadaiwa kughushi sahihi za ndugu zake katika kiapo, akionyesha ndugu hao wameridhia, fanye uhamisho wa umiliki wa ardhi, jambo ambalo sio kweli.

Salma ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Korogwe Mjini mwaka 2015 kwa tiketi ya ACT Wazalendo, akabiliwa na mashtaka matano yakiwemo ya kughushi sahihi za ndugu zake katika hati ya kiapo, kujipatia Sh1bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutokutii amri halali ya mahakama.

Mbali na Salma, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya jinai namba 101/2018 ni mwanasheria wa kujitegemea, Mohamed Majaliwa.

Gwaje ambaye ni shahidi wa nane katika kesi hiyo, alidai Machi 22, 2016, akiwa ofisi kwake Manispaa ya Ilala, alipokea nyaraka za kuhamisha umiliki wa ardhi kutoka kwa Salma.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi, Gwaje amedai nyaraka hizo zilizowasilisha katika Manispaa ya Ilala kwa ajili ya maombi ya kufanya uhamisho wa umiliki wa ardhi, zilikuwa na hati ya miliki halisi, mkataba wa mauziano  pamoja na kiapo.

"Nyaraka hizo zililetwa na mwaume ambaye alijitambulisha kuwa ni mwanasheria (Majaliwa) na zililetwa kwa lengo la kufanya uhamisho wa umiliki wa ardhi kutoka kwa Salma kwenda kwa Zahoro Salum" alidai Gwaje, ambaye ni anauzoefu wa miaka 10 sasa katika nafasi hiyo.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali, Daisy Makakala, shahidi huyo alidai Salma alikuwa anamiliki hati ya nyumba kwa niaba ya ndugu zake kwa sababu yeye ndio aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi.

Shahidi huyo alidai baada ya kuzipokea alizikagua na baada ya kujiridhisha aliziandikia kibali.

"Kabla ya kuziandikia kibali, nilimtaka Salma awasilishe kiapo kinachoonyesha warithi wengine kama wameridhia kuhamishwa kwa umiliki wa ardhi hiyo"

Baada ya kupata kibali, aliziandikia ada ya malipo kwa ajili ya kwenda kulipa Serikalini.

" Mteja anapomaliza kufanya malipo Serikalini, ndio huandaliwa kibali cha uhamisho ambacho kinatolewa na Ofisa Ardhi" alidai

Shaidi huyo alidai mmiliki wa ardhi ndio mtu sahihi wa kufanya maombi ya uhamisho wa umiliki wa ardhi.

Alieleza kwa mujibu wa utaratibu kutoka Wizara ya Ardhi, kama Msimamizi wa Mirathi anataka kufanya uhamisho wa umiliki wa ardhi,

lazima apeleke viapo vya warithi wenzake watatu, Manispaa husika.

Hata hivyo katika viapo hivyo vya warithi hao watatu, Salma alighushi sahihi za ndugu zake watatu, ambao ni Mhando Mtambo, Mboni Mtambo na Halima Mtambo, akionyesha kuwa ndugu hao walikubali kuhamisha umiliki wa ardhi, jambo ambalo sio kweli.

Hakimu Shaidi, baada ya kusikiliza ushahidi huo, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28, 2019 itakapoendelea na ushahidi.

Majaliwa yupo nje kwa dhamana, wakati Salma amerudishwa rumande kuendelea kutumikia kifungo chake cha miaka sita jela,  alichohukumiwa na mahakama hiyo, baada ya kupatikana na hatia ya  kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mbali na kifungo hicho, mahakama hiyo ilimuamuru Salma, kumlipa Ridhua Mringo kiasi cha Sh1 bilioni baada ya kuisababishia hasara

Hukumu hiyo ilitolewa Septemba 19, 2019 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Kelvin Mhina, baada ya mshtakiwa huyo kuitwa hatiani katika mashtaka 17 yakiwemo ya kuwasilisha nyaraka za uongo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kati ya mashtaka hayo 17; mashtaka 14 ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, huku matatu ni ya kutoa nyaraka za uongo.

Chanzo: mwananchi.co.tz