Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aeleza bunduki ilivyonunuliwa Kenya mauaji ya Bilionea Msuya

Bilionea Msuyaaaa Shahidi aeleza bunduki ilivyonunuliwa Kenya mauaji ya Bilionea Msuya

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Agosti 7, 2013 Jiji la Arusha na miji ya Moshi na Mirerani ilitikiswa na taarifa za kuuawa kwa kupigwa kwa risasi, mfanyabiashara maarufu wa madini, Erasto Msuya, tukio lililotokea wilayani Hai.

Katika tovuti yetu jana, tulikuletea ushahidi wa shahidi wa tano, sita na saba, ukiwamo ushahidi wa shahidi wa tano, Khalid Sankamunge ambaye ni mganga wa jadi, ambaye washitakiwa wawili kati ya saba walikwenda kwake kutafuta kinga. Alieleza Mahakama kuwa Septemba 9, 2013 akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Limbula, walifika vijana wawili aliowataja kuwa ni Karim Kihundwa (mshitakiwa wa tano) na Sadick Jabir (mshitakiwa wa sita), wakitaka awape dawa ya kinga.

Leo tunawaletea simulizi ya ushahidi wa shahidi wa nane wa Jamhuri, mkaguzi msaidizi wa Polisi, Herman Ngurukizi ambaye alikuwa ni miongoni mwa timu ya Intelijensia kufuatilia washukiwa wa mauaji.

Akiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Neema Mwanda kutoa ushahidi wake, Ngurukizi alisema Agosti 12, 2013 akiwa katika ofisi ya RCO Arusha, aliitwa na RCO Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi aliyekuwa Arusha.

Alimweleza kuwa siku hiyo asubuhi kuna mtuhumiwa aitwaye Mussa Juma Mangu (aliyekuwa mshitakiwa wa tatu) na katika mahojiano ya awali na polisi ameeleza tukio zima lilivyotokea, hivyo alimtaka kumhoji na kuandika maelezo yake.

Aliiomba Mahakama ikubali ayatoe maelezo hayo kama kielelezo, lakini mawakili wa upande wa utetezi walipinga na baada ya mabishano ya kisheria na kesi ndani ya kesi, Jaji Salma Maghimbi alikubali kuyapokea maelezo hayo.

Washitakiwa hawakuridhika na uamuzi huo na kuamua kuwasilisha notisi ya kukata rufaa mahakama ya Rufani, hata hivyo waliondoa kusudio lao hilo na kesi hiyo kuendelea kwa Inspekta Herman.

Kabla ya kuyasoma maelezo hayo, wakili wa Serikali mwandamizi, Abdalah Chavula ambaye ni mmoja wa mawakili wa Serikali waliokuwa wakiendesha kesi hiyo alimuongoza shahidi kuyatoa maelezo hayo kama kielelezo cha kesi.

Wakili Chavula: Ungependa maelezo hayo ya onyo ya Mussa Mangu yaingie mahakamani kama kielelezo cha kesi hii?

Shahidi: Ndiyo, ningependa yaingie kama kielelezo katika Mahakama yako tukufu.

Jaji Maghimbi: Statement (maelezo) hiyo inapokewa kama kielelezo P2.

Wakili Chavulla: Hebu tusomee hicho Mangu alichokuambia ukakiandika.

Shahidi: (akianza kuyasoma) maelezo yana kurasa 24 na niliyaandika 12/08/2013.

Laini za mipango zilivyosajiliwa

Katika maelezo hayo, mshitakiwa huyo alinukuliwa akisema bunduki iliyotumika kumuua Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya ilinunuliwa Namanga upande wa Kenya na mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed, kutoka kwa mtu mwenye asili ya Kisomali.

Katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo anaeleza kuwa yeye ni dereva wa mshtakiwa wa kwanza (Sharifu) anayemiliki migodi mitatu huko Mererani pamoja na magari manne na hoteli na kwa asilimia 100 ndiye alipanga mauaji.

Mangu alieleza anakumbuka Jumamosi moja, Sharifu alipeleka majina kwa mtu aliyemtaja ni Adamu ili akasajili laini za simu.

Mshtakiwa huyo anaeleza kuwa alimpelekea huyo Adamu majina hayo na ilipofika saa 12:00 jioni alimpigia simu ili amfuate kwa kuwa laini hizo tayari zilikuwa zimesajiliwa na alipomfuata alimkabidhi mbili za Airtel.

“Laini hizo alizipeleka nyumbani kwa Sharifu na kumkabidhi. Nakumbuka Julai 29, 2013 Sharifu alinipigia simu tena na kunielekeza niende kwa Adamu nikachukue laini nyingine mbili. Nilizichukua na kumpelekea Sharifu,” anaeleza.

Anaeleza kuwa, Agosti 3, 2013, alipigiwa simu na mshtakiwa wa kwanza na alipomfuata alimkuta akiwa na gari aina ya Toyota Noah.

Ndani ya gari hilo kulikuwa na vijana wawili, alimtaka aende na Adamu kumsaidia kununua pikipiki mbili, walizinunua kwa Sh3.4 milioni na kuzipeleka kwa Sharifu.

Pikipiki hizo zilisajiliwa kwa jina la Motii Ndoole ambalo ni jina lililotumika pia kusajili laini za simu ambazo Adamu aliagizwa azisajili na baadaye kukabidhiwa kwa mshtakiwa huyo wa kwanza.

Mshtakiwa huyo katika maelezo hayo anadai siku ya Jumanne ambayo tarehe haikumbuki, bosi wake alimwita katika hoteli yake ambako alimkuta na vijana watatu wakifanya mazungumzo.

“Alitoka ndani akiwa ameongozana na watu watatu nisiowafahamu. Mimi ndio niliendesha ile Noah wale vijana watatu wakawa wanaulizana nani akafanye naye biashara (Msuya),” anaeleza Mangu. “Nilimuuliza Sharifu (mshtakiwa wa kwanza) wanaenda kufanya biashara gani, akasema wanaenda kumuuzia mawe (madini ya Tanzanite) Erasto Msuya.”

Safari ya mauaji ilivyokuwa

Katika maelezo hayo, Mangu ananukuliwa akisema Agosti 7, 2013, mshitakiwa alikuja akiwa na gari aina ya Suzuki Vitara, ndani yake kulikuwa na wale vijana aliowakuta na bosi wake jana yake.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Mangu anasema bosi wake alimwelekeza aendeshe hiyo Suzuki Vitara kuelekea Moshi, lakini akawa anaongea na watu kwenye simu kuwa wamsubiri King’ori.

“Tulipofika King’ori, Sharifu alinielekeza nisimame mahali walipokuwa wamesimama vijana, wawili niliwatambua ni wale niliokutana nao jana yake,” anaeleza Mangu katika maelezo hayo.

Mangu katika maelezo hayo anaeleza watu hao wanne walikuwa na pikipiki mbili ambazo walizinunua jana yake na kuzipeleka nyumbani kwa Sharifu.

“Tulianza safari gari yetu ikiwa mbele huku pikipiki zikiwa nyuma. Tulielekea hadi kwenye miti ya mijohoro (Wilaya ya Hai) Sharifu aliniambia nisimamishe gari,” anaeleza Mangu.

Baada ya kusimamisha gari, ilikuja pikipiki nyekundu ambayo ni moja kati ya zile walizonunua na kuambiwa, “biashara ifanyikie hapa.”

Mangu anaeleza kuwa wao walirudi Arusha na kuwaacha vijana wale, lakini alipokuwa kijiweni siku hiyo hiyo saa 8:10 mchana alisikia taarifa kuwa Erasto (Msuya) amekufa kwa kupigwa risasi KIA.

Mshitakiwa huyo alipata picha vijana wale ndio waliofanya mauaji hayo kwa vile eneo la mauaji ndilo bosi wake aliwaambia wale vijana wafanyie biashara hapo.

Pia, anadai anaamini ndio waliohusika na mauaji hayo kwa vile jana yake, bosi wake alimweleza kuwa vijana wale wanakwenda kufanya biashara na Erasto na asubuhi yake aliona mfuko ukiwa na bunduki.

SMG ilivyonunuliwa Namanga

Katika maelezo ya nyongeza aliyoyaandika polisi, Mangu anaeleza kuwa Agosti 4, 2013, Sharifu alimwelekeza awapeleke watu ambao aliwatambua baadaye kwa majina ya Mredii (Shahibu) na Msoja hadi Namanga.

“Nilipack (kuegesha gari) upande wa Kenya. Mredii na Msoja walienda nisikokujua hadi saa 2:00 usiku waliporudi na kuniambia itabidi tulale Namanga kwa vile walichokifuata hawajakipata.

“Siku iliyofuata saa 4:00 asubuhi, Mredi alimpigia simu kwamba awafuate upande wa Kenya na alipowakuta walimwambia ampigie simu Sharifu kumjulisha kuwa ‘mzigo’ umepatikana,” anasema Mangu.

Hata hivyo, Mangu ananukuliwa akisema alikataa kumpigia simu bosi wake na ndipo Mredii alimpigia simu Sharifu na baadaye alimsikia akisema atatuma pesa kwa M-Pesa.

Mangu anadaiwa kukataa kubeba mzigo huo na ndipo Mredii akampigia simu Sharifu aje mwenyewe kubeba mzigo huo na wakati wanasubiri pale alikuja Msomali mmoja akawa anazungumza nao.

“Sharifu alikuja baada ya saa tatu. Mredii na yule msomali wakapanda kwenye gari la Sharifu. Nilihisi walichofuata Namanga ilikuwa ni bunduki lakini sikujua ni ya aina gani,” anaeleza Mangu.

Baada ya kumaliza kusoma maelezo hayo, ilifuata zamu ya mawakili wa utetezi kumhoji shahidi Ngurukizi, mahojiano kati ya wakili Hudson Ndusyepo anayemtetea Sharifu yalikuwa hivi.

Wakili Ndusyepo: Wakati unaandika maelezo ya mshtakiwa ulikuwa mji gani?

Shahidi: Nilikuwa Arusha.

Wakili Ndusyepo: Umeieleza Mahakama umepitia mafunzo mbalimbali, ulimwezesha mshtakiwa awasiliane na ndugu zake?

Shahidi: Alisema atatoa maelezo yake akiwa peke yake.

Wakili Ndusyepo: Ungemwezeshaje wakati ulikuwa ushapewa maelekezo na RCO kuwa kaandike maelezo yake?

Shahidi: Nilimweleza ana haki ya kuwa na wakili, ndugu, jamaa au rafiki lakini ningemwezeshaje wakati hataki?

Wakili Ndusyepo: Wakati RCO anakuambia kamchukue maelezo huyu anakiri kosa, kwa ufahamu wako lilikuwa ni kosa gani

Shahidi: Walichofanya na RCO siwezi kukizungumzia kwa sababu sikuwa sehemu ya mazungumzo yao.

Wakili Ndusyepo: Lakini katika ushahidi wako ulieleza baada ya RCO kumhoji ndio alikuita akakuambia huyu amekiri kosa uandike maelezo yake, si ndio?

Shahidi: Ufahamu wangu ni kumhoji na kuandika maelezo na ndicho nilichofanya.

Wakili Ndusyepo: Wewe kama askari mzoefu, unaieleza Mahakama kuwa alikiri, je alikiri kosa hilo la mauaji?

Shahidi: Nimesoma maelezo yake ya onyo aliyonieleza na chote alichokisema nimeeleza

Wakili Ndusyepo: Kwa hiyo kwa maelezo yako hakukiri kosa la mauaji

Shahidi: Yote aliyonieleza yako kwenye kielelezo. Mahakama itaona kama alikiri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live