Mshtakiwa wa tatu katika kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ameieleza mahakama kuwa alifungwa pingu na kuteswa kwa kuning’inizwa kichwa chini miguu juu baada ya kukamatwa Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mohamed Ling’wenya aliiambia Mahakama Kuu (Divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi) kuwa aliletewa maelezo ya onyo yaliyokwishaandikwa na kulazimishwa kusaini huku akitishiwa asiposaini yatamkuta yaliyompata akiwa Moshi.
Kesi dhidi ya Mbowe na wenzake iko katika hatua ya usikilizwaji wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi iliyoibuka baada ya mawakili wa utetezi kupinga maelezo ya onyo yanayodaiwa kuwa ya Ling’wenya yasipokewe mahakamani kama kielelezo cha ushahidi wa Jamhuri.
Upande wa mashtaka kupitia kwa shahidi wake wa nane katika kesi ya msingi uliiomba mahakama kuyapokea maelezo hayo, ili yawe kielelezo cha ushahidi.
Mawakili wa utetezi walipinga wakidai mshtakiwa huyo hajawahi kufikishwa kituo kikuu cha Polisi Dar anakodaiwa alitoa maelezo hayo alipokuwa amehifadhiwa.
Ifuatayo ni sehemu ya maelezo ya Ling’wenya alipoongozwa na wakili Dickson Matata kutoa ushahidi mbele ya Jaji Joachim Tiganga:-
“...nilikuwa askari wa Jeshi la Wananchi na niliacha mwaka 2017. Baada ya kuacha kazi nikawa naishi Shinyanga. Baadaye nikapata kazi Mtwara, nilikuwa kwenye kampuni ya Mhindi.
“Nilipoaacha huko nakumbuka nilipigiwa simu na Denis Urio kwamba Mbowe anahitaji ulinzi wa VIP Protection (ulinzi wa watu muhimu).
“Nikiwa Moshi Agosti 5, 2020 nilivamiwa na askari Polisi, nikawekwa kwenye gari na kupelekwa Central Police Moshi. Walipotuvamia hatukujua kama ni Polisi maana hawakujitambulisha. Baada ya kuingia kwenye gari na kufungwa pingu mmoja akatoa amri kwenda Central police.
“Nilikuwa na Adam Hassan Kasekwa (mshtakiwa wa pili). Baadhi ya waliotukamata akiwemo Goodluck Minja, Mahita, Jumanne, Ramadhani Kingai. Ndio hao nawakumbuka kwa majina.
“Baada ya kufikishwa Moshi niliwekwa selo na baada ya muda nikatolewa nikapelekwa kwenye chumba ambacho nilikuta watu wengi.
“Aliyekuwa ananihoji ni Jumanne na Mahita alikuwa anaandika, niliwajibu kilichonileta ni VIP protection kwa Mheshimiwa Mbowe, wao wakawa wanasema ‘sisi tunajua kilichokuleta huku, usitudanganye.’
“Baada ya kuniambia hivyo Mahita akasema ‘huyu si hataki kusema!’ Nilikuwa nimefungwa pingu, akanifunga na miguu, akachukua bomba akalipitisha katikati ya miguu, akanyanyua, nikabinuka, nyayo zikawa juu kichwa chini.
“Mahita akaanza kunipiga kwenye nyayo kama nusu saa hivi. Baadaye wakanifungua, kisha wakaninyanyua mpaka selo. Wakati napelekwa kuadhibiwa, Adam (mshtakiwa wa pili) alikuwa selo.
“Madai kuwa tulipofikishwa central police Moshi tulitoka tena na kuanza kuzunguka sehemu mbalimbali na polisi ni uongo, tulivyoingia hatukutoka mpaka tulipochukuliwa na kuanza safari.
“Wakati tuko kwenye gari kabla sijafungwa kitambaa walikuwemo kina Goodluck na wengine walioongezeka sikuwafahamu. “Njiani (kuelekea Dar es Salaam) hakuna kilichotokea ila mimi nilichoka shingo. Tulipofika nikiwa bado nimefungwa kitambaa, nikashushwa, nikainamishwa hivyo nikaingizwa selo.
Nilipotoa kitambaa niliposogea kwenye nondo nikaona kuna selo nyingine na kuna watu ambao walinisogelea na kuniuliza nini tatizo? Nikawaambia ‘nimekamatwa Moshi, sijui tatizo.’
“Yule mmoja akaniambia ‘hapa ni Tazara na wanaoletwa ni kwa tuhuma za kigaidi. Wakaniuliza ulikuwa unafanya kazi gani, ikamwambia ‘nilikuwa askari.’
“Naye akasema alikuwa askari kikosi cha kambi ya Twalipo kwa Aziz Ali, alikamatwa akiwa msikitini. Alikuwa ameiacha pikipiki yake nje na alipotoka akakuta imefungwa.
“Alipokamatwa hakujua ni suala gani, lakini akasema alishaambiwa ni ugaidi. Kisha akasogea mwingine akasema yeye ni Sheikh wa Manyara. Walikwenda kumchukua wakamwachia, wakamchukua tena.
“Baada ya muda nilikuja kutolewa selo, nikapanda juu na wakaingia watu ninaowafahamu - Alex Ahadi na Chum Chungulu - ambao walikuwa wa depo langu, nilikuwa nao 92 KJ.
“Baada ya muda akaingia Mahita, Jumanne, Goodluck, Kingai akaongezeka na mtu aliyeingia na video camera. Walikuwa wananihoji jinsi nilivyompata Mbowe, kilichonipeleka Moshi na nani aliyeniunganisha naye.
“Niliwajibu aliyeniunganisha ni Denis Urio ambaye ni Luteni wa Jeshi 92 KJ na kazi aliyokuwa ameniambia ni VIP protection. Kwa makadirio shughuli hiyo ya kunihoji dakika 30 hazifiki. Na aliniuliza sababu ya kwenda Moshi nikamwambia nilimfuata bosi ili tukaelewane naye.
“Tarehe 9, nilisikia mtu analia, nilipochungulia nikamtambua alikuwa ni Denis Urio ambaye nilishafanya naye kazi 92 KJ, kikosi cha Makomandoo.
“Sikuona walichokuwa wanamfanya ila niliona anatolewa kwa kuwa nilishasikia kilio. Kwa ufahamu wangu nilijua alikuwa anapigwa. Siku hiyo usiku nikafungwa kitambaa, nikaingizwa kwenye gari, tukaondoka. Selo alinitoa Goodluck na Mahita.
“Hiyo safari mwanzo sikuifahamu, wakati tunaendelea na safari Goodluck akanitikisa na bastola kuwa hapa nisilete ujanja na nikileta usumbufu watanipoteza.
“Tulipofika wao wakashuka na baada ya muda nikasikia sauti, mshushe huyu. Nikafunguliwa mlango nikashikwa kwenye suruali nyuma nikapelekwa kaunta nikafunguliwa kitambaa.
“Baadaye nilikuja kufahamu pale ni Mbweni baada ya kuuliza. Askari aliporudi akaanza kuniuliza particulars (taarifa) zangu. Tulivyoongea sana, baadaye akaniambia kama wewe ni komando basi mmeshafika watatu.
“Nikamuuliza huyo wa tatu ni nani, akaniambia mmoja nimeingia naye na mwingine ni Luteni wa jeshi. Nikamuuliza yukoje? Akaniambia ni mweupe, anaitwa Urio.
“Nikaingizwa kwenye chumba fulani hivi. Hicho chumba kutoka selo nilikokuwa nilitembea kwenye korido nikapishana na Urio.
Nilipokaa pale, Goodluck akawa amesimama mlangoni, akaja Jumanne na bahasha, akaifungua akasema bwana hatutaki usumbufu maana kila kitu tumeshakijua. Chukua hayo makaratasi usaini.
“Niliangalia mlango nikamuona Goodluck amesimama na bastola akaniambia ukitaka kuleta ujanja wako tutakufanya kama tulichokuwa Moshi. Niliogopa kwa mazingira yale ya bastola na wakati nafikiria pale kusaini akapitishwa Adam mimi nikiwa nimekaa na Jumanne.
“Zile karatasi alizotoa Jumanne sikupata kufahamu ni za nini. Hakunipa hata ruhusa ya kusoma, alichotaka ni kusaini tu. Aliziweka mezani nikasaini, akazirudisha tena kwenye bahasha.
“Tarehe 19, 2020 nikatolewa selo nikaingizwa kwenye gari, baadaye Adam naye akaletwa, tukaingizwa na tukaambiwa tusijali haki tutaipata Mahakamani,” alieleza mshtakiwa huyo.