Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aeleza alivyopewa ‘oda’ ya kumkamata Mdee akiwa kwa wazazi wake

11003 Shahidi+pic TanzaniaWeb

Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP) Batseba Kasanga ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alipokea ‘oda’ ya kumkamata Mbunge wa Kawe Halima Mdee nyumbani kwa wazazi wake kwa tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli.

Kasanga ambaye ni shahidi wa tatu wa mashtaka ameyasema hayo leo wakati akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Patrick Mwita.

Amesema alipofika nyumbani kwa wazazi wa Mdee eneo la Ubungo Kibangu, alipokewa na mama mzazi wa Mdee ambaye aliwaeleza wamsubiri kidogo Halima anajiandaa kwa kuwa alikuwa amepumzika kidogo.

Shahidi huyo amesema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Inadaiwa Julai 3, 2017 katika Makao Makuu Chadema, Mdee alitamka maneno ya kumkashfu Rais Magufuli yaliyosema

 “anaongea hovyohovyo, anatakiwa afungwe brek”.

Shahidi huyo amedai kuwa Julai 4, 2017 alipokea oda kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, Mark Njela aliyemtaka kwenda nyumbani kwa wazazi wa Mdee, Ubungo Kibangu ili kumkamata kwa tuhuma hizo.

Amedai kuwa walikwenda kwa kutumia gari la doria akisaidiana na askari wawili, walipofika walipokewa na kaka wa Halima ambaye aliwaelekeza kwa mama yao.

Kasanga amedai kuwa baada ya hapo Halima alitoka na wakamueleza kuwa wamekwenda kumkamata na kumpeleka Oysterbay Polisi na kwamba, wakati huo alikuwa yupo vizuri na baadhi ya ndugu zake walitoka wakaongozana nao kwenda kituoni hapo.

Amedai walipofika Oysterbay Polisi, Njela hakuwepo hivyo alimpigia simu na akamuelekeza amkabidhi Mdee kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala (RCO), Davis Msangi.

Shahidi huyo amedai kuwa baada ya kumkabidhi kwa Msangi aliondoka na kurudi kituoni kwake kuendelea na majukumu yake.

Hata hivyo alieleza kuwa yeye alikuwa hajawahi kumuona Mdee ana kwa ana na alikuwa akimsikia katika vyombo vya habari ikiwamo televisheni na magazeti.

Katika kesi hiyo, Mdee anatetewa na mawakili Peter Kibatala na Hekima Mwasipu.

Hekima alimuuliza shahidi huyo kuwa tangu tarehe aliyomkamata hadi sasa alishawahi kuyasikia maneno yaliyotamkwa na Halima Mdee.

Kasanga alijibu: “Kwa kweli sikuwahi kuyafuatilia.”

Kesi imeahirishwa hadi Septemba 11, 2018 saa nne asubuhi ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi.

Soma Zaidi:

Mkuu wa upelelezi akana kumhoji Rais Magufuli

Shahidi: Nilibaini maneno yaliyotamkwa na Halima Mdee ni jinai

Chanzo: mwananchi.co.tz