Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aeleza alivyokuta dawa za kulevya kabatini

51333 Pic+heroin

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Shahidi wa tatu katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin, inayomkabili mfanyabiashara Linna Muro (44), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jinsi alivyokuta dawa hizo, zikiwa zimezungushiwa karatasi ya nailoni na kuhifadhiwa nyuma ya kabati ya vyombo na katika meza vipodozi (dressingtable).

Shahidi huyo, Lubambe Kayumbu ambaye ni ofisa mkaguzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ameeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando, wakati akitoa ushahidi.

Alidai kuwa mbali na kukutwa na dawa hizo, Muro alikutwa na simu saba za mkononi ambapo simu tatu kati ya hizo ni aina ya Iphone pamoja hati mbili za kusafiria zenye majina yake.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Jenifer Massue, Kayumbu alidai kuwa Januari 24, 2018 alipata taarifa kutoka kwa msiri wake kuwa huko Tabata Bima katika nyumba za NSSF kuna mwanamke mmoja anajihusisha na dawa za kulevya.

“Baada ya taarifa hiyo, Januari 25, 2018, mimi na wenzangu sita tulienda katika nyumba ya Muro kwa ajili ya kufanya upekuzi,” amedai Kayumbu.

Shahidi huyo amedai kuwa baada ya kufika nyumbani kwa Muro, walimkuta mlinzi getini, aitwaye Riziki Simon ambapo walimuomba awaelekeze kwa mjumbe wa eneo hilo, aitwaye Walter Kagisa.

Amedai kuwa walivyofika kwa mjumbe huyo walieleza nia yao ya kwenda kufanya upekuzi katika nyumba ya Muro,  hivyo wanamuomba ili akashuhudie upekuzi huo.

“Tuliongozana na mjumbe hadi katika nyumba ya Muro na kujitambulisha kuwa sisi ni maofisa kutoka DCEA na kumuonyesha vitambulisho vyetu na kisha tukamueleza kuwa tunataka kufanya upekuzi katika nyumba yake kwa sababu anatuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya” amedai Kayumbu.

Walianza upekuzi katika chumba cha kulala ambapo walikuta pakiti mbili zilizokuwa zimefungwa kwa mfuko wa nailoni na kuhifadhiwa katika pochi ndogo (wallet) rangi nyekundu.

“Pia katika chumba hicho tulipata chupa ndogo moja ikiwa na kimiminika, hati mbili za kusafiria zenye majina ya Linna Muro, leseni tatu za biashara, laptop moja iliyokuwa mbovu na fedha taslimu Sh2,674,000” amedai shahidi.

Vile vile , walipata simu saba za mkononi, moderm ya zantel, mizani moja ya kupimia, pochi moja ndogo iliyokuwa na kadi za benki.

“Chumba cha pili, tulikuta pakiti ndogo ikiwa imezungushiwa pia nailoni ikiwa na unga unaodaiwa kuwa ni wa heroin na kwamba pochi hiyo ilikuwa juu ya meza ya vipodozi (dressing table)” amedai

Shahidi huyo, amedai pia walifanya upekuzi sebuleni na kukuta pakiti moja ya unga wa heroin ikiwa imezungushiwa karatasi, nyuma ya kabati la vyombo.

“Upelelezi huu ulianza usiku wa Januari 25, 2018 na kukamilika Januari 26, 2018 na mara baada ya kumaliza upekuzi huu, vitu vyote tulivyovikamata, tuliviorodhesha katika hati ya ukamataji na kisha kuondoka na mshtakiwa hadi katika ofisi zetu kwa ajili ya taratibu nyingine,” amedai Kayumbu.

kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho itakapoendelea na ushahidi na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Katika kesi ya msingi, Linna anakabiliwa na shtaka moja la kusafisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 43.95.

Anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 26, 2018 katika nyumba za Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) zilizopo Tabata Bima jijini Dar es Salaam.



Chanzo: mwananchi.co.tz