Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi adai mshtakiwa alijichoma kisu tumboni

Kisuu Shahidi adai mshtakiwa alijichoma kisu tumboni

Tue, 29 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa pili katika kesi ya kuua kwa kukusudia, Pudence Emmanuel (47) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa kuwa, mshtakiwa Diblo Saidi alijipeleka mwenyewe kituo cha Polisi Vingunguti na kisha kujichoma kisu tumboni hadi utumbo ukatoka nje.

Shahidi huyo ambaye ni Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, amedai kuwa mshtakiwa huyo alijichoma kisu mbele ya kituo hicho akiwa na nia ya kujiua baada ya kumfumania mke akiwa na mwanaume mwingine ndani ya nyumba yake.

Saidi anakabiliwa na shtaka moja la kumuua mke wake aitwaye Herieth Justine kwa kumchoma na kisu tumboni, begani na kifuani, baada ya kumfumania na mwanaume mwingine.

Emmanuel ambaye kwa sasa yupo ofisi ya Upelelezi na Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ameieleza mahakama hiyo, leo Novemba 28, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi aliyepewa Mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi hiyo.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali Aziza Mhina, shahidi huyo amedai kuwa Machi 11, 2018, alipokea simu kutoka aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Kipolisi Buguruni, Davis Msangi aende Vingunguti kuna mwanamke mmoja amechomwa kisu kifuani na begani.

"Wakati nataka kuondoka kuelekea Vingunguti nilipokea simu kutoka kwa Sajenti Martine kuwa kuna tukio jingine la mwananume kujichoma kisu nje ya kituo cha Polisi Vingunguti ndipo nilipoamua kwenda kituo cha Polisi Vingunguti kulipotokea tukio la kujichoma kisu," amedai Mkaguzi Emmanuel na kuongoza

"Baada ya kufika pale tulimkuta mwanaume aliyefahamika kwa jina la Diblo akiwa amejichoma kisu cha tumbo na utumbo ulikuwa umetoka nje.

“Ndipo Sajenti Martine alinieleza kuwa mwanaume huyo alikuwa anaingia kituo cha polisi kabla hajaingia ndani alisema anajiua kutokana na kumfumania mkewe na walipomchukua na kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu," amedai Shahidi.

Pudence amendelea kudai kuwa baada ya kumpeleka Diblo Hospitali, waliamua kwenda eneo kulikofanyika tukio la tukio la mauaji ya Herieth kwa ajili kufanya uchunguzi.

"Katika uchunguzi wetu tuligundua Herieth ana majeraha ya kisu sehemu ya bega, kifuani na tumboni vyote vikiwa upande wa kushoto ndipo tukipoamuru achukuliwe na apelekwe hospitali ya Muhimbili," amedai.

Amedai baada ya kutoa maelekezo hayo, alikuja mwanaume aliyetambulika kwa jina la Castor na kueleza kuwa yule Diblo ndio aliyemchoma kisu Herieth.

"Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa Herieth alifariki dunia muda mrefu baada ya kuvuja damu nyingi.

“Uchunguzi uliofanywa na jopo la madaktari ulibaini kuwa licha ya Diblo kujichoma kisu hadi utumbo kutoka nje, alikuwa bado hajafariki na hivyo kuanzishiwa matibabu akiwa chini ya uangalizi wa polisi," amedai Emmanuel.

Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, ameulizwa maswali na mshitakiwa huyo na moja ya maswali hayo ni kuwa aliwezaje kumkumbuka Diblo kwani tangu tukio hilo la mauaji tangu litokee hadi ni miaka mitano imepita.

Akijibu swali hiyo, Emmanuel amedai kuwa tukio la mauaji ya Herieth lilikuwa ni tukio kubwa na limeacha kumbukumbu katika akili yake kwa kuwa alikuta damu ambazo hawai kuziona eneo la tukio.

"Mheshimiwa hakimu hata hapa ninapotoa ushahidi sura ya Herieth naiona kwa hiyo ni tukio kubwa ambalo siwezi kulisahau," amedai Shahidi.

Shahidi baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Kyaruzi ameahirisha kesi hiyo hadi kesho, Novemba 29, 2022 itakapoendelea na ushahidi na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa , Machi 11, 2018 katika eneo la Vingunguti alimuua kwa makusudi Herieth Justine, baada ya kudai kuwa amemfumania na mwanaume mwingine ndani ya nyumba yake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live